56
Wokovu Kwa Ajili Ya Wengine 
 
1 Hili ndilo asemalo Bwana:  
“Dumisheni haki  
na mkatende lile lililo sawa,  
kwa maana wokovu wangu u karibu  
na haki yangu itafunuliwa upesi.   
2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,  
mtu yule alishikaye kwa uthabiti,  
yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,  
auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”   
   
 
3 Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme,  
“Hakika Bwana atanitenga na watu wake.”  
Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,  
“Mimi ni mti mkavu tu.”   
4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:  
“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,  
ambao huchagua kile kinachonipendeza  
na kulishika sana agano langu:   
5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake  
kumbukumbu na jina bora  
kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:  
nitawapa jina lidumulo milele,  
ambalo halitakatiliwa mbali.   
6 Wageni wanaoambatana na Bwana  
ili kumtumikia,  
kulipenda jina la Bwana,  
na kumwabudu yeye,  
wote washikao Sabato bila kuinajisi  
na ambao hushika sana agano langu:   
7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu  
na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.  
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao  
zitakubalika juu ya madhabahu yangu;  
kwa maana nyumba yangu itaitwa  
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”   
8 Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye  
Waisraeli waliohamishwa:  
“Bado nitawakusanya wengine kwao  
zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”   
Mashtaka Ya Mungu Dhidi Ya Waovu 
 
9 Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni,  
njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!   
10 Walinzi wa Israeli ni vipofu,  
wote wamepungukiwa na maarifa;  
wote ni mbwa walio bubu,  
hawawezi kubweka;  
hulala na kuota ndoto,  
hupenda kulala.   
11 Ni mbwa wenye tamaa kubwa,  
kamwe hawatosheki.  
Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu;  
wote wamegeukia njia yao wenyewe,  
kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.   
12 Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo!  
Tunywe kileo sana!  
Kesho itakuwa kama leo,  
au hata bora zaidi.”