65
Hukumu Na Wokovu
“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia.
Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.
Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu,
nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’
Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu
kwa watu wakaidi,
wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri,
wafuatao mawazo yao wenyewe:
taifa ambalo daima hunikasirisha
machoni pangu,
wakitoa dhabihu katika bustani
na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;
watu waketio katikati ya makaburi
na kukesha mahali pa siri,
walao nyama za nguruwe,
nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,
wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie,
kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’
Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu,
ni moto uwakao mchana kutwa.
 
“Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu:
sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu;
nitalipiza mapajani mwao:
dhambi zenu na dhambi za baba zenu,”
asema Bwana.
“Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima
na kunichokoza mimi juu ya vilima,
nitawapimia mapajani mwao
malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”
Hili ndilo asemalo Bwana:
“Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana
katika kishada cha zabibu,
nao watu husema, ‘Usikiharibu,
kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’
hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu;
sitawaangamiza wote.
Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo,
na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu,
nao watu wangu wateule watairithi,
nako huko wataishi watumishi wangu.
10 Sharoni itakuwa malisho
kwa ajili ya makundi ya kondoo,
na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia
kwa makundi ya ngʼombe,
kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.
 
11 “Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana
na kuusahau mlima wangu mtakatifu,
ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati,*
na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa
kwa ajili ya Ajali,
12 nitawaagiza mfe kwa upanga,
nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa;
kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika,
nilisema lakini hamkusikiliza.
Mlitenda maovu machoni pangu,
nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”
13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:
“Watumishi wangu watakula,
lakini ninyi mtaona njaa;
watumishi wangu watakunywa
lakini ninyi mtaona kiu;
watumishi wangu watafurahi,
lakini ninyi mtaona haya.
14 Watumishi wangu wataimba
kwa furaha ya mioyo yao,
lakini ninyi mtalia
kutokana na uchungu wa moyoni,
na kupiga yowe kwa sababu
ya uchungu wa roho zenu.
15 Mtaliacha jina lenu
kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa;
Bwana Mwenyezi atawaua ninyi,
lakini watumishi wake atawapa jina jingine.
16 Yeye aombaye baraka katika nchi
atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli;
yeye aapaye katika nchi
ataapa kwa Mungu wa kweli.
Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika
na kufichwa kutoka machoni pangu.
Mbingu Mpya Na Dunia Mpya
17 “Tazama, nitaumba
mbingu mpya na dunia mpya.
Mambo ya zamani hayatakumbukwa,
wala hayatakuja akilini.
18 Lakini furahini na kushangilia daima
katika hivi nitakavyoumba,
kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,
nao watu wake wawe furaha.
19 Nami nitaifurahia Yerusalemu
na kuwafurahia watu wangu;
sauti ya maombolezo na ya kilio
haitasikika humo tena.
 
20 “Kamwe hatakuwepo tena ndani yake
mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu,
au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake.
Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja
atahesabiwa kwamba ni kijana tu,
yeye ambaye hatafika miaka mia moja,
atahesabiwa kuwa amelaaniwa.
21 Watajenga nyumba na kuishi ndani yake;
watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.
22 Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake,
au kupanda mazao na wengine wale.
Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti,
ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu,
wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi
kazi za mikono yao.
23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure,
wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga,
kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Bwana,
wao na wazao wao pamoja nao.
24 Kabla hawajaita, nitajibu,
nao wakiwa katika kunena, nitasikia.
25 Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja,
naye simba atakula nyasi kama maksai,
lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka.
Hawatadhuru wala kuharibu
katika mlima wangu mtakatifu wote,”
asema Bwana.
* 65:11 Bahati alikuwa mungu wa Wakaldayo ambaye pia alijulikana kama Gadi. 65:11 Ajali au Meni alikuwa mungu wa majaliwa.