66
Hukumu Na Matumaini
1 Hili ndilo asemalo Bwana,
“Mbingu ni kiti changu cha enzi,
nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.
Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu?
Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
2 Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote,
hivyo vikapata kuwepo?”
asema Bwana.
“Mtu huyu ndiye ninayemthamini:
yeye ambaye ni mnyenyekevu
na mwenye roho yenye toba,
atetemekaye asikiapo neno langu.
3 Lakini yeyote atoaye dhabihu ya fahali
ni kama yeye auaye mtu,
na yeyote atoaye sadaka ya mwana-kondoo,
ni kama yule avunjaye shingo ya mbwa.
Yeyote atoaye sadaka ya nafaka,
ni kama yule aletaye damu ya nguruwe,
na yeyote afukizaye uvumba wa kumbukumbu,
ni kama yule aabuduye sanamu.
Wamejichagulia njia zao wenyewe,
nazo nafsi zao zinafurahia machukizo yao.
4 Hivyo, mimi pia nitawachagulia mapigo makali,
nami nitaleta juu yao kile wanachokiogopa.
Kwa maana nilipoita, hakuna yeyote aliyejibu,
niliposema, hakuna yeyote aliyesikiliza.
Walifanya maovu machoni pangu
na kuchagua lile linalonichukiza.”
5 Sikieni neno la Bwana,
ninyi mtetemekao kwa neno lake:
“Ndugu zenu wanaowachukia ninyi
na kuwatenga ninyi kwa sababu ya Jina langu, wamesema,
‘Bwana na atukuzwe,
ili tupate kuona furaha yenu!’
Hata sasa wataaibika.
6 Sikieni hizo ghasia kutoka mjini,
sikieni hizo kelele kutoka hekaluni!
Ni sauti ya Bwana ikiwalipa adui zake
yote wanayostahili.
7 “Kabla hajasikia utungu, alizaa;
kabla hajapata maumivu,
alizaa mtoto mwanaume.
8 Ni nani amepata kusikia jambo kama hili?
Ni nani amepata kuona mambo kama haya?
Je, nchi yaweza kuzaliwa kwa siku moja,
au taifa laweza kutokea mara?
Mara Sayuni alipoona utungu,
alizaa watoto wake.
9 Je, nilete mwana hadi wakati wa kuzaliwa
na nisizalishe?” asema Bwana.
“Je, nifunge tumbo la uzazi
wakati mimi ndiye nizalishaye?”
asema Mungu wako.
10 “Shangilieni pamoja na Yerusalemu na mfurahi kwa ajili yake,
ninyi nyote mnaompenda,
shangilieni kwa nguvu pamoja naye,
ninyi nyote mnaoomboleza juu yake.
11 Kwa kuwa mtanyonya na kutosheka
katika faraja ya matiti yake;
mtakunywa sana,
na kuufurahia wingi wa mafuriko ya ustawi wake.”
12 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Nitamwongezea amani kama mto,
nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho;
utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake
na kubembelezwa magotini pake.
13 Kama mama anavyomfariji mtoto wake,
ndivyo nitakavyokufariji wewe,
nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”
14 Wakati mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia,
nanyi mtastawi kama majani;
mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake,
bali ghadhabu yake kali
itaonyeshwa kwa adui zake.
15 Tazama, Bwana anakuja na moto,
magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli,
atateremsha hasira yake kwa ghadhabu kali,
na karipio lake pamoja na miali ya moto.
16 Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake
Bwana atatekeleza hukumu juu ya watu wote,
nao wengi watakuwa ni wale
waliouawa na Bwana.
17 “Watu wote wanaojiweka wakfu na kujitakasa wenyewe ili kwenda bustanini, wakimfuata aliye katikati ya wale ambao hula nyama za nguruwe na panya pamoja na vitu vingine vilivyo machukizo, watafikia mwisho wao pamoja,” asema Bwana.
18 “Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.
19 “Nitaweka ishara katikati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia juu ya sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa.
20 Nao watawaleta ndugu zenu wote, kutoka mataifa yote, mpaka kwenye mlima wangu mtakatifu katika Yerusalemu kama sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, katika magari ya vita na magari makubwa, juu ya nyumbu na ngamia,” asema Bwana. “Watawaleta, kama Waisraeli waletavyo sadaka zao za nafaka, katika Hekalu la Bwana, katika vyombo safi kwa kufuata desturi za ibada.
21 Nami nitachagua baadhi yao pia wawe makuhani na Walawi,” asema Bwana.
22 “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Bwana, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu.
23 Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Bwana.
24 “Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi. Funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”