10
Tarumbeta Za Fedha
Bwana akamwambia Mose: “Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka. Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania. Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako. Wakati mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka. Ukisikika mlio wa pili wa jinsi hiyo, walioko kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka. Ili kukusanya kusanyiko, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.
“Wana wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo. Wakati mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Bwana Mungu wenu na kuokolewa kutoka kwa adui zenu. 10 Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Waisraeli Waondoka Sinai
11 Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya maskani ya Ushuhuda. 12 Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine mpaka wingu lilipotua katika Jangwa la Parani. 13 Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Bwana kupitia kwa Mose.
14 Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya alama yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao. 15 Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari, 16 naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni. 17 Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.
18 Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya alama yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao. 19 Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni, 20 naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi. 21 Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilikuwa isimamishwe kabla wao hawajafika.
22 Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya alama yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao. 23 Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase, 24 naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.
25 Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya alama yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao. 26 Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri, 27 naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali. 28 Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.
29 Basi Mose akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Mose, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo Bwana amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja nasi tutakutendea mema, kwa maana Bwana ameahidi mambo mema kwa Israeli.”
30 Akajibu, “Hapana, sitakwenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.”
31 Lakini Mose akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali ambapo yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu. 32 Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na Bwana.”
33 Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Bwana, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Bwana liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. 34 Wingu la Bwana lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
35 Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Mose alisema,
“Ee Bwana, inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako.”
36 Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,
“Ee Bwana, rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”