9
Pasaka Huko Sinai
Bwana akasema na Mose katika Jangwa la Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri. Akasema, “Waamuru Waisraeli waadhimishe Pasaka katika wakati ulioamriwa. Adhimisheni wakati ulioamriwa, yaani wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi huu, kufuatana na desturi zake zote na masharti yake.”
Hivyo Mose akawaambia Waisraeli waiadhimishe Pasaka, nao wakafanya hivyo kwenye Jangwa la Sinai wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Waisraeli wakafanya kila kitu kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
Lakini baadhi yao hawakuweza kuadhimisha Pasaka siku ile kwa sababu walikuwa najisi kwa taratibu za kiibada kwa ajili ya kugusa maiti. Kwa hiyo wakamwendea Mose na Aroni siku ile ile, wakamwambia Mose, “Tumekuwa najisi kwa sababu tumegusa maiti, lakini kwa nini tuzuiliwe kumtolea Bwana sadaka yake pamoja na Waisraeli wengine katika wakati ulioamriwa?”
Mose akawajibu, “Ngojeni mpaka nitafute kile Bwana anachoagiza kuwahusu ninyi.”
Ndipo Bwana akamwambia Mose, 10 “Waambie Waisraeli: ‘Wakati mmoja wenu au wazao wenu wanapokuwa najisi kwa sababu ya maiti au wakiwa safarini, hata hivyo wanaweza kuadhimisha Pasaka ya Bwana. 11 Wataiadhimisha wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Watamla mwana-kondoo, pamoja na mkate usiotiwa chachu, na mboga chungu. 12 Wasibakize chochote hadi asubuhi wala wasivunje mifupa ya mwana-kondoo. Wakati wanapoadhimisha Pasaka, hawana budi kufuata masharti yote. 13 Lakini kama mtu ni safi kwa taratibu za kiibada naye hayuko safarini, asipoadhimisha Pasaka, mtu huyo hana budi kukatiliwa mbali na watu wake kwa sababu hakutoa sadaka ya Bwana kwa wakati ulioamriwa. Mtu huyo atawajibika kubeba matokeo ya dhambi yake.
14 “ ‘Mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana, lazima afanye hivyo kwa kufuata desturi na masharti. Lazima masharti yawe sawasawa kwa mgeni na mzawa.’ ”
Wingu La Moto Juu Ya Maskani
(Kutoka 40:34-38)
15 Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni mpaka asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto. 16 Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto. 17 Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu liliposimama, Waisraeli walipiga kambi. 18 Kwa amri ya Bwana Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu liliposimama juu ya Maskani, Waisraeli walibaki wamepiga kambi.
19 Wakati wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya Bwana nao hawakuondoka. 20 Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya Bwana wangelipiga kambi na kisha kwa amri yake wangeliondoka. 21 Wakati mwingine wingu lilikuwepo kuanzia jioni mpaka asubuhi tu, na lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Ikiwa ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka. 22 Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka.
23 Kwa amri ya Bwana walipiga kambi, na kwa amri ya Bwana waliondoka. Walitii amri ya Bwana, kufuatana na agizo lake kupitia Mose.