5
Utakaso Wa Kambi
Bwana akamwambia Mose, “Waamuru Waisraeli kumtoa nje ya kambi mtu yeyote ambaye ana ugonjwa wa ngozi uambukizao,* au anayetokwa na majimaji ya aina yoyote, au ambaye ni najisi kwa utaratibu wa ibada kwa sababu ya maiti. Hii itakuwa ni kwa wote, yaani, wanaume na wanawake; watoeni nje ya kambi ili wasije wakanajisi kambi yao, ambamo ninaishi miongoni mwao.” Waisraeli wakafanya hivyo; wakawatoa nje ya kambi. Wakafanya kama vile Bwana alivyokuwa amemwelekeza Mose.
Malipo Kwa Ajili Ya Makosa
Bwana akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Wakati mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Bwana, mtu huyo ana hatia, na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea. Lakini ikiwa mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye malipo yanaweza kufanywa kwa ajili ya kosa, malipo yatakuwa mali ya Bwana, nayo ni lazima apewe kuhani, pamoja na kondoo dume ambaye anatumika kufanyia upatanisho kwa ajili yake. Matoleo yote matakatifu ya Waisraeli wanayoleta kwa kuhani yatakuwa yake. 10 Kila kitu cha mtu kilichowekwa wakfu ni chake mwenyewe, lakini kile atoacho kwa kuhani kitakuwa cha kuhani.’ ”
Jaribio Kwa Ajili Ya Mke Asiye Mwaminifu
11 Kisha Bwana akamwambia Mose, 12 “Nena na Waisraeli uwaambie: ‘Ikiwa mke wa mtu amepotoka na si mwaminifu kwa mumewe, 13 kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine, tendo hili likafichika kwa mumewe na unajisi wake usigundulike (kwa kuwa hakuna ushahidi dhidi yake, naye hakukamatwa katika tendo hilo), 14 nazo hisia za wivu zikamjia mumewe na kumshuku mkewe, naye mke yule ni najisi, au mumewe ana wivu na akamshuku ingawa si najisi, 15 basi atampeleka mkewe kwa kuhani. Huyo mume itampasa apeleke pia sadaka ya unga wa shayiri kiasi cha sehemu ya kumi ya efa kwa niaba ya mkewe. Huyo mwanaume kamwe asimimine mafuta juu ya huo unga wala asiweke uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, sadaka ya ukumbusho ili kukumbushia uovu.
16 “ ‘Kuhani atamleta huyo mwanamke na kumsimamisha mbele za Bwana. 17 Kisha kuhani atachukua sehemu ya maji matakatifu ndani ya gudulia la udongo na kuchanganya na baadhi ya vumbi kutoka sakafu ya Maskani. 18 Baada ya kuhani kumsimamisha huyo mwanamke mbele za Bwana, atazifungua nywele za huyo mwanamke na kuweka sadaka ya ukumbusho mikononi mwake, ile sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, huku kuhani mwenyewe akishikilia yale maji machungu yaletayo laana. 19 Kisha kuhani atamwapiza huyo mwanamke, akimwambia, “Ikiwa hakuna mwanaume mwingine aliyekutana kimwili nawe, wala hujapotoka na kuwa najisi wakati ukiwa umeolewa na mumeo, maji haya machungu yaletayo laana na yasikudhuru. 20 Lakini ikiwa umepotoka wakati ukiwa umeolewa na mume wako na umejinajisi mwenyewe kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine asiyekuwa mumeo”; 21 hapa kuhani atamweka huyo mwanamke chini ya laana ya kiapo akisema: “Bwana na awafanye watu wako wakulaani na kukukataa, wakati Bwana atakapolifanya paja lako kupooza na tumbo lako kuvimba. 22 Maji haya yaletayo laana na yaingie ndani ya mwili wako ili tumbo lako livimbe na paja lako lipooze.”
“ ‘Kisha mwanamke atasema, “Amen. Iwe hivyo.”
23 “ ‘Kuhani ataandika laana hizi kwenye kitabu, kisha atazioshea laana hizo kwenye yale maji machungu. 24 Kuhani atamnywesha yule mwanamke yale maji machungu yaletayo laana, nayo maji haya yatamwingia na kumsababishia maumivu makali. 25 Kuhani atachukua sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu kutoka mikononi mwa huyo mwanamke, naye ataipunga mbele za Bwana na kuileta madhabahuni. 26 Kisha kuhani atachota sadaka ya nafaka mkono uliojaa kama sehemu ya kumbukumbu na kuiteketeza juu ya madhabahu, baada ya hayo, atamtaka huyo mwanamke anywe yale maji. 27 Kama amejitia unajisi na kukosa uaminifu kwa mumewe, wakati anapotakiwa anywe maji yale yaletayo laana, yatamwingia na kusababisha maumivu makali; tumbo lake litavimba na paja lake litapooza, naye atakuwa amelaaniwa miongoni mwa watu wake. 28 Hata hivyo, ikiwa huyo mwanamke hakujitia unajisi, naye ni safi, atasafishwa hatia na ataweza kuzaa watoto.
29 “ ‘Basi, hii ndiyo sheria ya wivu mwanamke anapopotoka na kujitia unajisi akiwa ameolewa na mumewe, 30 au hisia za wivu zinapomjia mwanaume kwa sababu ya kumshuku mkewe. Kuhani atamfanya huyo mwanamke kusimama mbele za Bwana na atatumia sheria hii yote kwa huyo mwanamke. 31 Mume atakuwa hana hatia ya kosa lolote, bali mwanamke atayachukua matokeo ya dhambi yake.’ ”
* 5:2 Ugonjwa wa ngozi uambukizao hapa ina maana ya ukoma. 5:15 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja. 5:22 Paja lipooze hapa ina maana ya kuwa tasa au kuharibu mimba.