6
Mnadhiri
Bwana akamwambia Mose, “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Bwana kama Mnadhiri, ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu. Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.
“ ‘Kwa muda wote wa nadhiri yake ya kujitenga kwa ajili ya Bwana, wembe hautapita kichwani mwake. Ni lazima awe mtakatifu mpaka kipindi cha kujitenga kwake kwa ajili ya Bwana kiishe; ni lazima aache nywele za kichwa chake zirefuke. Kwa kipindi chochote cha kujitenga kwa ajili ya Bwana hatakaribia maiti. Hata kama baba yake mwenyewe au mama au kaka au dada akifa, hatajinajisi mwenyewe kwa taratibu za ibada kwa ajili yao, kwa sababu ishara ya kujiweka wakfu kwake kwa Mungu ipo katika kichwa chake. Kwa kipindi chote cha kujitenga kwake yeye ni wakfu kwa Bwana.
“ ‘Kama mtu yeyote akifa ghafula karibu naye, atakuwa ametiwa unajisi nywele zake alizoziweka wakfu, hivyo ni lazima anyoe nywele zake siku ya utakaso wake, yaani siku ya saba. 10 Kisha siku ya nane ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa kuhani katika mlango wa Hema la Kukutania. 11 Kuhani atatoa mmoja kama sadaka ya dhambi, na mwingine kama sadaka ya kuteketezwa ili kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa sababu ametenda dhambi kwa kuwepo mbele ya maiti. Siku iyo hiyo atakiweka wakfu kichwa chake. 12 Ni lazima ajitoe kabisa kwa Bwana kwa kipindi cha kujitenga kwake, na ni lazima atoe mwana-kondoo wa mwaka mmoja kama sadaka ya hatia. Siku zilizopita hazitahesabiwa kwa sababu alijitia unajisi katika siku zake za kujitenga.
13 “ ‘Basi hii ndiyo sheria kwa ajili ya Mnadhiri baada ya kipindi chake cha kujitenga kupita. Ataletwa kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 14 Hapo atatoa sadaka zake kwa Bwana: yaani, mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kondoo mke wa mwaka mmoja asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo dume asiye na waa kwa ajili ya sadaka ya amani, 15 pamoja na sadaka zake za nafaka na za vinywaji, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, yaani maandazi yaliyotengenezwa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta, na mikate myembamba iliyopakwa mafuta.
16 “ ‘Kuhani atavileta vitu hivyo mbele za Bwana na kufanya sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa. 17 Ataleta pia kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, na atatoa dhabihu kondoo dume kama sadaka ya amani kwa Bwana, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka ya kinywaji.
18 “ ‘Kisha kwenye ingilio la Hema la Kukutania, Mnadhiri ni lazima anyoe nywele zake ambazo alikuwa ameziweka wakfu. Atazichukua hizo nywele na kuziweka ndani ya moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka ya amani.
19 “ ‘Baada ya Mnadhiri kunyoa hizo nywele zake za kujitenga kwake, kuhani atampa mikononi mwake bega la kondoo dume lililochemshwa, na pia andazi na mkate mwembamba kutoka kwenye kikapu, vyote vikiwa vimetengenezwa bila kuwekwa chachu. 20 Kisha kuhani ataviinua mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.
21 “ ‘Hii ndiyo sheria ya Mnadhiri ambaye anaweka nadhiri kwa matoleo yake kwa Bwana kufuatana na kujitenga kwake, zaidi ya chochote kile anachoweza kupata. Ni lazima atimize nadhiri aliyoiweka kufuatana na sheria ya Mnadhiri.’ ”
Baraka Ya Kikuhani
22  Bwana akamwambia Mose, 23 “Mwambie Aroni na wanawe, ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni:
24 “ ‘ “Bwana akubariki
na kukulinda;
25  Bwana akuangazie nuru ya uso wake
na kukufadhili;
26  Bwana akugeuzie uso wake
na kukupa amani.” ’
27 “Hivyo wataliweka Jina langu juu ya Waisraeli, nami nitawabariki.”