Zaburi 101
Ahadi Ya Kuishi Kwa Uadilifu Na Kwa Haki
Zaburi ya Daudi.
Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako;
kwako wewe, Ee Bwana, nitaimba sifa.
Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama:
utakuja kwangu lini?
 
Nitatembea nyumbani mwangu
kwa moyo usio na lawama.
Sitaweka mbele ya macho yangu
kitu kiovu.
 
Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani;
hawatashikamana nami.
Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami;
nitajitenga na kila ubaya.
 
Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri,
huyo nitamnyamazisha;
mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi
huyo sitamvumilia.
 
Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,
ili waweze kuishi pamoja nami;
yeye ambaye moyo wake hauna lawama
atanitumikia.
 
Mdanganyifu hatakaa
nyumbani mwangu,
yeye asemaye kwa uongo
hatasimama mbele yangu.
 
Kila asubuhi nitawanyamazisha
waovu wote katika nchi;
nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya
kutoka mji wa Bwana.