KITABU CHA TANO
107
(Zaburi 107–150)
Kumsifu Mungu Kwa Wema Wake
Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema,
upendo wake wadumu milele.
Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi,
wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,
wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,
kutoka mashariki na magharibi,
kutoka kaskazini na kusini.
 
Baadhi yao walitangatanga jangwani,
hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.
Walikuwa na njaa na kiu,
nafsi zao zikadhoofika.
Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
Akawaongoza kwa njia iliyo sawa
hadi mji ambao wangeweza kuishi.
Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,
na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.
 
10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu,
wafungwa wakiteseka katika minyororo,
11 kwa sababu walikuwa wameasi
dhidi ya maneno ya Mungu
na kudharau shauri
la Aliye Juu Sana.
12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu;
walijikwaa na hapakuwepo yeyote wa kuwasaidia.
13 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu
na akavunja minyororo yao.
15 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba
na kukata mapingo ya chuma.
 
17 Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao,
wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.
18 Wakachukia kabisa vyakula vyote,
wakakaribia malango ya mauti.
19 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
20 Akalituma neno lake na kuwaponya,
akawaokoa kutoka maangamizo yao.
21 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
22 Na watoe dhabihu za kushukuru,
na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.
 
23 Wengine walisafiri baharini kwa meli,
walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.
24 Waliziona kazi za Bwana,
matendo yake ya ajabu kilindini.
25 Kwa maana alisema na kuamsha tufani
iliyoinua mawimbi juu.
26 Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini,
katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.
27 Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi,
ujanja wao ukafikia ukomo.
28 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawatoa kwenye taabu yao.
29 Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono,
mawimbi ya bahari yakatulia.
30 Walifurahi ilipokuwa shwari,
naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.
31 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu,
na wamsifu katika baraza la wazee.
 
33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa,
chemchemi za maji zitiririkazo kuwa ardhi yenye kiu,
34 nchi izaayo ikawa ya chumvi isiyofaa,
kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.
35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji,
nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zitiririkazo;
36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo,
nao wakajenga mji wangeweza kuishi.
37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu,
nayo ikazaa matunda mengi,
38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana,
wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.
 
39 Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa
kwa kuonewa, maafa na huzuni.
40 Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu,
aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.
41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao,
na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.
42 Wanyofu wataona na kufurahi,
lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.
 
43 Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya,
na atafakari upendo mkuu wa Bwana.