Zaburi 108
Kuomba Msaada Dhidi Ya Adui
(Zaburi 57:7-11; 60:5-12)
Wimbo. Zaburi ya Daudi.
Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;
nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu;
uaminifu wako unazifikia anga.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
 
Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
Mungu amenena kutoka patakatifu pake:
“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi
na kulipima Bonde la Sukothi.
Gileadi ni yangu, Manase ni yangu,
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
Moabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
 
10 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
11 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,
na hutoki tena na majeshi yetu?
12 Tuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.