Zaburi 110
Bwana Na Mfalme Wake Mteule
Zaburi ya Daudi.
1 Bwana amwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
mpaka nitakapowafanya adui zako
kuwa mahali pa kuweka miguu yako.”
2 Bwana ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni;
utatawala katikati ya adui zako.
3 Askari wako watajitolea kwa hiari
katika siku yako ya vita.
Ukiwa umevikwa fahari takatifu,
kutoka tumbo la mapambazuko
utapokea umande wa ujana wako.
4 Bwana ameapa,
naye hatabadilisha mawazo yake:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.”
5 Bwana yuko mkono wako wa kuume,
atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake.
6 Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga
na kuwaponda watawala wa dunia nzima.
7 Atakunywa maji katika kijito kando ya njia,
kwa hiyo atainua kichwa chake juu.