*
Zaburi 111
Sifa Za Bwana Kwa Matendo Ya Ajabu
Msifuni Bwana.
 
Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote,
katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.
 
Kazi za Bwana ni kuu,
wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.
Kazi zake zimejaa fahari na utukufu,
haki yake hudumu daima.
Amefanya maajabu yake yakumbukwe,
Bwana ni mwenye neema na huruma.
Huwapa chakula wale wanaomcha,
hulikumbuka agano lake milele.
Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake,
akiwapa nchi za mataifa mengine.
Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki,
mausia yake yote ni ya kuaminika.
Zinadumu milele na milele,
zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.
Aliwapa watu wake ukombozi,
aliamuru agano lake milele:
jina lake ni takatifu na la kuogopwa.
 
10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,
wote wanaozifuata amri zake wana busara.
Sifa zake zadumu milele.
* Zaburi 111: Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.