Zaburi 114
Maajabu Ya Mungu Wakati Israeli Walipotoka Misri
Wakati Israeli walipotoka Misri,
nyumba ya Yakobo kutoka kwa watu wa lugha ngeni,
Yuda alifanywa makao matakatifu ya Mungu,
Israeli akawa milki yake.
 
Bahari ilitazama ikakimbia,
Yordani ulirudi nyuma,
milima ilirukaruka kama kondoo dume,
vilima kama wana-kondoo.
 
Ee bahari, ni nini kilichokufanya ukakimbia,
nawe, ee Yordani, ukarudi nyuma,
enyi milima mkarukaruka kama kondoo dume,
enyi vilima, kama wana-kondoo?
 
Ee dunia, tetemeka mbele za Bwana,
mbele za Mungu wa Yakobo,
aliyegeuza mwamba kuwa dimbwi la maji,
mwamba mgumu kuwa chemchemi za maji.