Zaburi 116
Shukrani Kwa Kuokolewa Kutoka Mauti
1 Ninampenda Bwana kwa maana amesikia sauti yangu;
amesikia kilio changu ili anihurumie.
2 Kwa sababu amenitegea sikio lake,
nitamwita siku zote za maisha yangu.
3 Kamba za mauti zilinizunguka,
maumivu makuu ya kuzimu yalinipata,
nikalemewa na taabu na huzuni.
4 Ndipo nikaliitia jina la Bwana:
“Ee Bwana, niokoe!”
5 Bwana ni mwenye neema na haki,
Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
6 Bwana huwalinda wanyenyekevu,
nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
7 Ee nafsi yangu, tulia tena,
kwa kuwa Bwana amekuwa mwema kwako.
8 Kwa kuwa wewe, Ee Bwana,
umeniokoa nafsi yangu na mauti,
macho yangu kutokana na machozi,
miguu yangu kutokana na kujikwaa,
9 ili niweze kutembea mbele za Bwana,
katika nchi ya walio hai.
10 Niliamini, kwa hiyo nilisema,
“Mimi nimeteseka sana.”
11 Katika taabu yangu nilisema,
“Wanadamu wote ni waongo.”
12 Nimrudishie Bwana nini
kwa wema wake wote alionitendea?
13 Nitakiinua kikombe cha wokovu
na kulitangaza jina la Bwana.
14 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana
mbele za watu wake wote.
15 Kifo cha watakatifu kina thamani
machoni pa Bwana.
16 Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
mimi ni mtumishi wako,
mwana wa mjakazi wako;
umeniweka huru
toka katika minyororo yangu.
17 Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru
na kuliita jina la Bwana.
18 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana
mbele za watu wake wote,
19 katika nyua za nyumba ya Bwana,
katikati yako, ee Yerusalemu.
Msifuni Bwana.