Zaburi 122
Sifa Kwa Yerusalemu
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
Nilishangilia pamoja na wale walioniambia,
“Twende nyumbani ya Bwana.”
Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama
malangoni mwako.
 
Yerusalemu imejengwa vyema kama mji
ambao umeshikamanishwa pamoja.
Huko ndiko makabila hukwea,
makabila ya Bwana,
kulisifu jina la Bwana kulingana na maagizo
waliopewa Israeli.
Huko viti vya enzi vya hukumu hukaa,
viti vya enzi vya nyumba ya Daudi.
 
Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu:
“Wote wakupendao na wawe salama.
Amani na iwepo ndani ya kuta zako
na usalama ndani ya ngome zako.”
Kwa ajili ya ndugu zangu na marafiki,
nitasema, “Amani iwe ndani yako.”
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana Mungu wetu,
nitatafuta mafanikio yako.