Zaburi 124
Shukrani Kwa Ukombozi Wa Israeli
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
Kama Bwana asingalikuwa upande wetu;
Israeli na aseme sasa:
kama Bwana asingalikuwa upande wetu,
wakati watu walipotushambulia,
wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu,
wangalitumeza tungali hai,
mafuriko yangalitugharikisha,
maji mengi yangalitufunika,
maji yaendayo kasi
yangalituchukua.
 
Bwana asifiwe,
yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
Tumeponyoka kama ndege
kutoka mtego wa mwindaji;
mtego umevunjika,
nasi tukaokoka.
Msaada wetu ni katika jina la Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.