Zaburi 125
Usalama Wa Watu Wa Mungu
Wimbo wa kwenda juu.
Wale wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni,
ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele.
Kama milima inavyozunguka Yerusalemu,
ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake
sasa na hata milele.
 
Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi
waliopewa wenye haki,
ili wenye haki wasije wakatumia
mikono yao kutenda ubaya.
 
Ee Bwana, watendee mema walio wema,
wale walio wanyofu wa moyo.
Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka,
Bwana atawafukuza pamoja na watenda mabaya.
 
Amani iwe juu ya Israeli.