Zaburi 146
Kumsifu Mungu Mwokozi
1 Msifuni Bwana!
Ee nafsi yangu, umsifu Bwana,
2 Nitamsifu Bwana maisha yangu yote;
nitamwimbia Mungu wangu sifa
wakati wote niishipo.
3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu,
kwa wanadamu ambao hufa,
ambao hawawezi kuokoa.
4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini,
siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.
5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake,
6 Muumba wa mbingu na nchi,
na bahari na vyote vilivyomo ndani yake:
Bwana anayedumu kuwa mwaminifu
milele na milele.
7 Naye huwapatia haki walioonewa
na kuwapa wenye njaa chakula.
Bwana huwaweka wafungwa huru,
8 Bwana huwafumbua vipofu macho,
Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao,
Bwana huwapenda wenye haki.
9 Bwana huwalinda wageni
na kuwategemeza yatima na wajane,
lakini hupinga njia za waovu.
10 Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, ee Sayuni,
kwa vizazi vyote.
Msifuni Bwana.