Zaburi 147
Kumsifu Mungu Mwenye Nguvu Zote
Msifuni Bwana.
 
Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa,
jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!
 
Bwana hujenga Yerusalemu,
huwakusanya Israeli walio uhamishoni.
Anawaponya waliovunjika mioyo
na kuvifunga vidonda vyao.
 
Huzihesabu nyota
na huipa kila moja jina lake.
Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,
ufahamu wake hauna kikomo.
Bwana huwahifadhi wanyenyekevu
lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini.
 
Mwimbieni Bwana kwa shukrani,
mpigieni Mungu wetu kinubi.
Yeye huzifunika anga kwa mawingu,
huinyeshea ardhi mvua,
na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima.
Huwapa chakula mifugo
na pia makinda ya kunguru yanapolia.
 
10 Furaha yake haipo katika nguvu za farasi,
wala furaha yake kwenye miguu ya mwanadamu.
11  Bwana hupendezwa na wale wamchao,
wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.
 
12 Mtukuze Bwana, ee Yerusalemu,
msifu Mungu wako, ee Sayuni,
13 kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako
na huwabariki watu wako walio ndani yako.
14 Huwapa amani mipakani mwenu
na kukushibisha kwa ngano safi kabisa.
 
15 Hutuma amri yake duniani,
neno lake hukimbia kasi.
16 Anatandaza theluji kama sufu
na kutawanya umande kama majivu.
17 Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe.
Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake?
18 Hutuma neno lake na kuviyeyusha,
huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka.
 
19 Amemfunulia Yakobo neno lake,
sheria zake na maagizo yake kwa Israeli.
20 Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote,
hawazijui sheria zake.
 
Msifuni Bwana.