Zaburi 149
Wimbo Wa Kumsifu Mungu Kwa Wema Wake
Msifuni Bwana.
 
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.
 
Israeli na washangilie katika Muumba wao,
watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao.
Na walisifu jina lake kwa kucheza
na wampigie muziki kwa matari na kinubi.
Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake,
anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu.
Watakatifu washangilie katika heshima hii,
na waimbe kwa shangwe vitandani mwao.
 
Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao
na upanga ukatao kuwili mikononi mwao,
ili walipize mataifa kisasi
na adhabu juu ya mataifa,
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,
wakuu wao kwa pingu za chuma,
ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao.
Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote.
 
Msifuni Bwana.