Zaburi 15
Kitu Mungu Anachotaka
Zaburi ya Daudi.
Bwana, ni nani awezaye kukaa
katika Hekalu lako?
Nani awezaye kuishi
katika mlima wako mtakatifu?
 
Ni yule aendaye pasipo mawaa,
atendaye yaliyo haki,
asemaye kweli toka moyoni mwake,
na hana masingizio ulimini mwake,
asiyemtenda jirani yake vibaya,
na asiyemsingizia mwenzake,
ambaye humdharau mtu mbaya,
lakini huwaheshimu wale wamwogopao Bwana,
yule atunzaye kiapo chake
hata kama anaumia.
Yeye akopeshaye fedha yake bila riba,
na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia.
 
Mtu afanyaye haya
kamwe hatatikisika.