Zaburi 14
Uovu Wa Wanadamu
(Zaburi 53)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Mpumbavu anasema moyoni mwake,
“Hakuna Mungu.”
Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa;
hakuna hata mmoja atendaye mema.
 
Bwana anawachungulia wanadamu chini
kutoka mbinguni
aone kama wako wenye akili,
wowote wanaomtafuta Mungu.
Wote wamepotoka,
wameharibika wote pamoja,
hakuna atendaye mema.
Naam, hakuna hata mmoja!
 
Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza:
wale ambao huwala watu wangu
kama watu walavyo mkate,
hao ambao hawamwiti Bwana?
Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu,
maana Mungu yupo pamoja na wenye haki.
Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini,
bali Bwana ndiye kimbilio lao.
 
Laiti wokovu wa Israeli
ungalikuja kutoka Sayuni!
Wakati Bwana arejeshapo
wafungwa wa watu wake,
Yakobo na ashangilie,
Israeli na afurahi!