Zaburi 23
Bwana Mchungaji Wetu
Zaburi ya Daudi.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
Hunilaza katika malisho
ya majani mabichi,
kando ya maji matulivu huniongoza,
hunihuisha nafsi yangu.
Huniongoza katika njia za haki
kwa ajili ya jina lake.
Hata kama nikipita katikati
ya bonde la uvuli wa mauti,
sitaogopa mabaya,
kwa maana wewe upo pamoja nami;
fimbo yako na mkongojo wako
vyanifariji.
 
Waandaa meza mbele yangu
machoni pa adui zangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
kikombe changu kinafurika.
Hakika wema na upendo vitanifuata
siku zote za maisha yangu,
nami nitakaa nyumbani mwa Bwana
milele.