Zaburi 55
Maombi Ya Mtu Aliyesalitiwa Na Rafiki
Kwa mwimbishaji. Na ala za uimbaji. Utenzi wa Daudi.
Ee Mungu, sikiliza maombi yangu,
wala usidharau hoja yangu.
Nisikie na unijibu.
Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa
kwa sauti ya adui,
kwa kukaziwa macho na waovu,
kwa sababu wananiletea mateso juu yangu
na kunitukana kwa hasira zao.
 
Moyo wangu umejaa uchungu,
hofu ya kifo imenishambulia.
Woga na kutetemeka vimenizunguka,
hofu kuu imenigharikisha.
Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa!
Ningeruka niende mbali kupumzika.
Ningalitorokea mbali sana
na kukaa jangwani,
ningaliharakisha kwenda mahali pa salama,
mbali na tufani kali na dhoruba.”
 
Ee Bwana, uwatahayarishe waovu
na uwachanganyishie semi zao,
maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.
10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake,
uovu na dhuluma vimo ndani yake.
11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini,
vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.
 
12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia,
kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,
ningejificha asinione.
13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,
mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri,
tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.
 
15 Kifo na kiwajie adui zangu ghafula,
na washuke kuzimu wangali hai,
kwa maana uovu upo ndani yao.
 
16 Lakini ninamwita Mungu,
naye Bwana huniokoa.
17 Jioni, asubuhi na adhuhuri
ninalia kwa huzuni,
naye husikia sauti yangu.
18 Huniokoa nikawa salama katika vita
vilivyopangwa dhidi yangu,
ingawa watu wengi hunipinga.
19 Mungu anayemiliki milele,
atawasikia na kuwaadhibu,
watu ambao hawabadilishi njia zao,
wala hawana hofu ya Mungu.
 
20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake,
naye huvunja agano lake.
21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi,
hata hivyo vita vimo moyoni mwake.
Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,
hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.
 
22 Mtwike Bwana fadhaa zako,
naye atakutegemeza,
hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.
23 Lakini wewe, Ee Mungu,
utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.
Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,
hawataishi nusu ya siku zao.
 
Lakini mimi ninakutumaini wewe.