Zaburi 56
Kumtumaini Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.
Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;
mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,
wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
 
Wakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
 
Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu,
siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.
Wananifanyia hila, wanajificha,
wanatazama hatua zangu,
wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
 
Wasiepuke kwa vyovyote,
Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
Andika maombolezo yangu,
orodhesha machozi yangu katika gombo lako:
je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
 
Ndipo adui zangu watarudi nyuma
ninapoita msaada.
Kwa hili nitajua kwamba Mungu
yuko upande wangu.
10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu,
11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
 
12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako,
nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti
na miguu yangu kwenye kujikwaa,
ili niweze kuenenda mbele za Mungu
katika nuru ya uzima.