Zaburi 6
Sala Kwa Ajili Ya Msaada Wakati Wa Taabu
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako,
wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.
2 Unirehemu Bwana,
kwa maana nimedhoofika;
Ee Bwana, uniponye,
kwa maana mifupa yangu
ina maumivu makali.
3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi.
Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini?
4 Geuka Ee Bwana, unikomboe,
uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.
5 Hakuna mtu anayekukumbuka
akiwa amekufa.
Ni nani awezaye kukusifu
akiwa kuzimu?
6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni;
usiku kucha nafurikisha
kitanda changu kwa machozi;
nimelowesha viti vyangu vya fahari
kwa machozi.
7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika,
yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.
8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya,
kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu.
9 Bwana amesikia kilio changu kwa huruma,
Bwana amekubali sala yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika,
watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.