Zaburi 77
Matendo Makuu Ya Mungu Yanakumbukwa
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu.
Nilimlilia Mungu ili anisaidie,
nilimlilia Mungu ili anisikie.
Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana,
usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka
na nafsi yangu ilikataa kufarijika.
 
Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni;
nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.
Ulizuia macho yangu kufumba;
nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.
Nilitafakari juu ya siku zilizopita,
miaka mingi iliyopita,
nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku.
Moyo wangu ulitafakari
na roho yangu ikauliza:
 
“Je, Bwana atakataa milele?
Je, hatatenda mema tena?
Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele?
Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?
Je, Mungu amesahau kuwa na huruma?
Je, katika hasira amezuia huruma yake?”
 
10 Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu:
lakini nitakumbuka
miaka ya mkono wa kuume
wa Aliye Juu Sana.”
11 Nitayakumbuka matendo ya Bwana;
naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.
12 Nitazitafakari kazi zako zote
na kuyawaza matendo yako makuu.
 
13 Ee Mungu, njia zako ni takatifu.
Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza,
umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa.
15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako,
uzao wa Yakobo na Yosefu.
 
16 Maji yalikuona, Ee Mungu,
maji yalikuona yakakimbia,
vilindi vilitetemeka.
17 Mawingu yalimwaga maji,
mbingu zikatoa ngurumo kwa radi,
mishale yako ikametameta huku na huko.
18 Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli,
umeme wako wa radi ukaangaza dunia,
nchi ikatetemeka na kutikisika.
19 Njia yako ilipita baharini,
mapito yako kwenye maji makuu,
ingawa nyayo zako hazikuonekana.
 
20 Uliongoza watu wako kama kundi
kwa mkono wa Mose na Aroni.