Zaburi 8
Utukufu Wa Mungu Na Heshima Ya Mwanadamu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi.
Ee Bwana, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
 
Umeuweka utukufu wako
juu ya mbingu.
Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao
umeamuru sifa,
kwa sababu ya watesi wako,
kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
 
Nikiziangalia mbingu zako,
kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota,
ulizoziratibisha,
mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,
binadamu ni nani hata unamjali?
Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,
ukamvika taji ya utukufu na heshima.
 
Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
Mifugo na makundi yote pia,
naam, na wanyama wa kondeni,
ndege wa angani na samaki wa baharini,
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
 
Ee Bwana, Bwana wetu,
tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!