Zaburi 84
Kuionea Shauku Nyumba Ya Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora.
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
makao yako yapendeza kama nini!
Nafsi yangu inatamani sana,
naam, hata kuona shauku,
kwa ajili ya nyua za Bwana;
moyo wangu na mwili wangu
vinamlilia Mungu Aliye Hai.
 
Hata shomoro amejipatia makao,
mbayuwayu amejipatia kiota
mahali awezapo kuweka makinda yake:
mahali karibu na madhabahu yako,
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wanaokusifu wewe daima.
 
Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
Wanapopita katika Bonde la Baka,*
hulifanya mahali pa chemchemi,
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.
Huendelea toka nguvu hadi nguvu,
hadi kila mmoja afikapo
mbele za Mungu huko Sayuni.
 
Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu;
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
Ee Mungu, uitazame ngao yetu,
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
 
10 Siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu
kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao,
Bwana hutoa wema na heshima;
hakuna kitu chema anachowanyima
wale ambao hawana hatia.
 
12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.
* Zaburi 84:6 Yaani Bonde la Vilio. Zaburi 84:6 Au: baraka.