Zaburi 85
Maombi Kwa Ajili Ya Ustawi Wa Taifa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.
Ee Bwana, ulionyesha wema kwa nchi yako.
Ulimrejeshea Yakobo baraka zake.*
Ulisamehe uovu wa watu wako,
na kufunika dhambi zao zote.
Uliweka kando ghadhabu yako yote
na umegeuka na kuiacha hasira yako kali.
 
Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena,
nawe uiondoe chuki yako juu yetu.
Je, utatukasirikia milele?
Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote?
Je, hutatuhuisha tena,
ili watu wako wakufurahie?
Utuonyeshe upendo wako usiokoma, Ee Bwana,
utupe wokovu wako.
 
Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Bwana;
anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake:
lakini nao wasirudie upumbavu.
Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao,
ili utukufu wake udumu katika nchi yetu.
 
10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja,
haki na amani hubusiana.
11 Uaminifu huchipua kutoka nchi,
haki hutazama chini kutoka mbinguni.
12 Naam, hakika Bwana atatoa kilicho chema,
nayo nchi yetu itazaa mavuno yake.
13 Haki itatangulia mbele yake
na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake.
* Zaburi 85:1 Au: Uliwarudisha mateka wa Yakobo.