Zaburi 87
Sifa Za Yerusalemu
Zaburi ya wana wa Kora. Wimbo.
Ameuweka msingi wake katika mlima mtakatifu;
Bwana anayapenda malango ya Sayuni
kuliko makao yote ya Yakobo.
Mambo matukufu yanasemwa juu yako,
ee mji wa Mungu:
“Nitaweka kumbukumbu ya Rahabu* na Babeli
miongoni mwa wale wanaonikubali mimi:
Ufilisti pia na Tiro, pamoja na Kushi,
nami nitasema, ‘Huyu alizaliwa Sayuni.’ ”
 
Kuhusu Sayuni itasemwa hivi,
“Huyu na yule walizaliwa humo,
naye Aliye Juu Sana mwenyewe
atamwimarisha.”
Bwana ataandika katika orodha ya mataifa:
“Huyu alizaliwa Sayuni.”
Watakapokuwa wanapiga vinanda wataimba,
“Chemchemi zangu zote ziko kwako.”
* Zaburi 87:4 Rahabu hapa ni jina la ushairi la Misri. Zaburi 87:4 Kushi hapa ina maana ya Naili ya juu, yaani Ethiopia.