Zaburi 91
Mungu Mlinzi Wetu
Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,
atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.*
Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”
 
Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,
na maradhi ya kuambukiza ya kuua.
Atakufunika kwa manyoya yake,
chini ya mbawa zake utapata kimbilio,
uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.
Hutaogopa vitisho vya usiku,
wala mshale urukao mchana,
wala maradhi ya kuambukiza
yanayonyemelea gizani,
wala tauni iharibuyo adhuhuri.
Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,
kumi elfu mkono wako wa kuume,
lakini haitakukaribia wewe.
Utatazama tu kwa macho yako
na kuona adhabu ya waovu.
 
Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako:
naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,
10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe,
hakuna maafa yataikaribia hema yako.
11 Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako,
wakulinde katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuinua,
ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka wakali,
simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.
 
14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;
nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.
15 Ataniita, nami nitamjibu;
nitakuwa pamoja naye katika taabu,
nitamwokoa na kumheshimu.
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha
na kumwonyesha wokovu wangu.”
* Zaburi 91:1 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.