32
Senakeribu Aitishia Yerusalemu
(2 Wafalme 18:13-37; 19:14-19, 35-37; Isaya 36:1-22; 37:8-38)
Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizunguka miji yenye ngome kwa jeshi, akifikiri kuiteka iwe yake. Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu, akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?” Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwepo na kuimarisha Milo* katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.
Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya: “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
Hatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzunguka Lakishi, akawatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda, na kwa watu wote wa Yuda waliokuwako humo, kusema:
10 “Hili ndilo asemalo Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mmeweka tumaini lenu wapi, hata mnaendelea kukaa katika Yerusalemu, hali mmezungukwa na jeshi? 11 Hezekia asemapo, ‘Bwana Mungu wetu atatuokoa kutokana na mkono wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, naye atawaacha mfe kwa njaa na kiu. 12 Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?
13 “Je, hamjui yale mimi na baba zangu tuliyoyafanya kwa mataifa yote ya nchi zingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu? 14 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza ameweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mungu wenu kuwaokoa mkononi mwangu? 15 Sasa basi, msikubali Hezekia awadanganye na kuwapotosha namna hii. Msimwamini, kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lolote wala wa ufalme wowote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”
16 Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi ya Bwana aliye Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia. 17 Mfalme pia aliandika barua akimtukana Bwana, Mungu wa Israeli na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.” 18 Kisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji. 19 Wakanena juu ya Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena juu ya miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.
20 Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili. 21 Naye Bwana akamtuma malaika ambaye aliangamiza wanajeshi wote, na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, mfalme wa Ashuru akarudi nchini mwake kwa aibu. Naye alipokwenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake wakamuua kwa upanga.
22 Hivyo Bwana akamwokoa Hezekia na watu wa Yerusalemu kutoka mkononi mwa Senakeribu mfalme wa Ashuru na kutoka mikononi mwa wengine wote. Bwana akawastarehesha kila upande. 23 Watu wengi wakaleta sadaka Yerusalemu kwa ajili ya Bwana na zawadi za thamani kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda. Tangu hapo na kuendelea, Hezekia aliheshimiwa sana na mataifa yote.
Kiburi Cha Hezekia, Mafanikio Na Kifo
(2 Wafalme 20:1-3, 12-19; Isaya 38:1-3; 39:1-8)
24 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Akamwomba Bwana, ambaye alimjibu na kumpa ishara. 25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonyesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu. 26 Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana haikuja juu yao katika siku za Hezekia.
27 Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezi, ngao na aina zote za vyombo vya thamani. 28 Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta. Akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo, na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi. 29 Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ngʼombe kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana.
30 Ilikuwa ni Hezekia aliyeziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya. 31 Lakini wakati wajumbe walipotumwa na watawala wa Babeli kumuuliza juu ya ishara ambayo ilitokea katika nchi, Mungu alimwacha ili kumjaribu na kujua kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.
32 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia na matendo yake ya kujitoa kwa moyo yameandikwa katika maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi kwenye kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 33 Hezekia akalala na baba zake na akazikwa kwenye kilima mahali yalipo makaburi ya wazao wa Daudi. Yuda wote na watu wa Yerusalemu wakamheshimu alipofariki. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.
* 32:5 Milo maana yake Boma la Ngome.