33
Manase Mfalme Wa Yuda
(2 Wafalme 21:1-18)
1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na mitano.
2 Akafanya maovu machoni pa Bwana, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli.
3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa, pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu.
4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Bwana ambamo Bwana alikuwa amesema, “Jina langu litadumu Yerusalemu milele.”
5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Bwana akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani.
6 Akawatoa wanawe kuwa kafara kwa kuwapitisha katika moto katika Bonde la Ben-Hinomu, akafanya ulozi, uaguzi na uchawi, akataka ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa Bwana, akaichochea hasira yake.
7 Akachukua ile sanamu aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu la Mungu ambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele.
8 Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Mose.”
9 Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Bwana aliwaangamiza mbele ya Waisraeli.
10 Bwana akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali.
11 Hivyo Bwana akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
12 Katika dhiki yake akamsihi Bwana Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.
13 Naye alipomwomba, Bwana akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza kilio chake, kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba Bwana ndiye Mungu.
14 Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli, pia akaufanya kuwa mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.
15 Akaondolea mbali miungu ya kigeni na kuondoa sanamu kutoka Hekalu la Bwana pamoja na madhabahu zote alizozijenga katika kile kilima kilichojengwa Hekalu na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.
16 Kisha akarudisha madhabahu ya Bwana na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie Bwana, Mungu wa Israeli.
17 Lakini hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia miungu, lakini wakimtolea Bwana Mungu wao peke yake.
18 Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
19 Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa kwake uaminifu pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia miungu, kule kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake, yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji.
20 Manase akalala pamoja na baba zake akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Amoni Mfalme Wa Yuda
(2 Wafalme 21:19-26)
21 Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili, alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili.
22 Akatenda maovu machoni mwa Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase.
23 Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele za Bwana, badala yake Amoni aliongeza hatia zaidi na zaidi.
24 Watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, nao wakamuulia kwake nyumbani.
25 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.