5
1 Hivyo Solomoni alipomaliza kazi ya Hekalu la Bwana, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: yaani, fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la Mungu.
Sanduku La Agano Laletwa Hekaluni
(1 Wafalme 8:1-9)
2 Kisha Solomoni akawaita huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Bwana kutoka Sayuni, Mji wa Daudi.
3 Nao wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa mfalme wakati wa sikukuu mwezi wa saba.
4 Wazee wote wa Israeli walipofika, Walawi wakajitwika Sanduku la Agano,
5 nao wakalipandisha Sanduku na Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani, waliokuwa Walawi, walivibeba vitu hivyo,
6 naye Mfalme Solomoni na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ngʼombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa.
7 Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Bwana hadi mahali pake ndani ya sehemu takatifu ndani ya Hekalu, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi.
8 Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kufunika Sanduku na mipiko yake ya kubebea.
9 Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilizojitokeza kutoka kwenye Sanduku, nazo zilionekana ukiwa mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo.
10 Ndani ya Sanduku hapakuwepo kitu kingine chochote isipokuwa zile mbao mbili ambazo Mose alikuwa ameziweka ndani yake huko Horebu, mahali ambapo Bwana alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
11 Basi makuhani wakaondoka hapo Mahali Patakatifu. Makuhani wote waliokuwa huko walikuwa wamejiweka wakfu, bila kujali migawanyo yao.
12 Walawi wote waliokuwa waimbaji, yaani, Asafu, Hemani, Yeduthuni, wana wa ndugu zao, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu, wakiwa wamevaa kitani safi huku wakipiga matoazi, vinubi na zeze. Walikuwa pamoja na makuhani 120 wakipiga tarumbeta.
13 Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Bwana, nao alipoinua sauti zao pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Bwana wakisema:
“Yeye ni mwema;
upendo wake unadumu milele.”
Ndipo Hekalu la Bwana likajazwa na wingu,
14 nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu la Mungu.