12
Maadui Wa Yerusalemu Kuangamizwa
1 Hili ni neno la Bwana kuhusu Israeli. Bwana, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema:
2 “Nitakwenda kufanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbisha mataifa yote yanayoizunguka. Yuda utazingirwa kwa vita na Yerusalemu pia.
3 Katika siku hiyo, wakati mataifa yote ya dunia yatakapokusanyika dhidi yake, nitaufanya Yerusalemu kuwa jabali lisilosogezwa kwa mataifa yote. Wote watakaojaribu kulisogeza watajiumiza wenyewe.
4 Katika siku hiyo nitampiga kila farasi kwa hofu ya ghafula, naye ampandaye nitampiga kwa uwazimu,” asema Bwana. “Nitalielekeza jicho langu la ulinzi juu ya nyumba ya Yuda, nami nitawapofusha farasi wote wa mataifa.
5 Kisha viongozi wa Yuda watasema mioyoni mwao, ‘Watu wa Yerusalemu wana nguvu kwa sababu Bwana Mwenye Nguvu Zote ni Mungu wao.’
6 “Katika siku hiyo nitawafanya viongozi wa Yuda kuwa kama kigae cha moto ndani ya lundo la kuni, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watateketeza kulia na kushoto mataifa yote yanayowazunguka, lakini Yerusalemu utabaki salama mahali pake.
7 “Bwana atayaokoa makao ya Yuda kwanza, ili heshima ya nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu isiwe kubwa zaidi kuliko ile ya Yuda.
8 Katika siku hiyo, Bwana atawakinga wale waishio Yerusalemu, ili kwamba aliye dhaifu kupita wote miongoni mwao awe kama Daudi, nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama Malaika wa Bwana akiwatangulia.
9 Katika siku hiyo nitatoka kuangamiza mataifa yote yatakayoshambulia Yerusalemu.
Kumwombolezea Yule Aliyechomwa Mkuki
10 “Nami nitamiminia nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu roho ya neema na maombi. Watanitazama mimi, yule waliyemchoma. Nao watamwombolezea kama mtu anayemwombolezea mwanawe wa pekee na kusikitika kwa uchungu kama anayemsikitikia mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.
11 Katika siku hiyo kilio kitakuwa kikubwa Yerusalemu, kama kilio cha Hadad-Rimoni katika tambarare ya Megido.
12 Nchi itaomboleza, kila ukoo peke yake, nao wake zao peke yao. Ukoo wa nyumba ya Daudi na wake zao, ukoo wa nyumba ya Nathani na wake zao,
13 ukoo wa nyumba ya Lawi na wake zao, ukoo wa Shimei na wake zao,
14 na koo zote zilizobaki na wake zao.