13
Kutakaswa Dhambi
1 “Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi.
2 “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi.
3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.
4 “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu.
5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’
6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’
Mchungaji Apigwa, Nao Kondoo Watawanyika
7 “Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu,
dhidi ya mtu aliye karibu nami!”
asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
“Mpige mchungaji,
nao kondoo watatawanyika,
nami nitageuza mkono wangu
dhidi ya walio wadogo,
8 katika nchi yote,” asema Bwana,
“theluthi mbili watapigwa na kuangamia;
hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake.
9 Hii theluthi moja nitaileta katika moto;
nitawasafisha kama fedha isafishwavyo
na kuwajaribu kama dhahabu.
Wataliitia Jina langu
nami nitawajibu;
nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’
nao watasema, ‘Bwana ni Mungu wetu.’ ”