16
Paulo pia alipokuja Derbe na Lystra; na tazama, pale palikuwepo na mwanafunzi aitwaye Timotheo, ni Kijana aliyezaliwa na mama wa Kiyahudi ambaye ni muumini na baba yake ni Mgiriki. Watu wa Listra na Ikonia walimshudia vizuri. Paulo alimtaka ili asafiri naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwako huko kwani wote walimjua kuwa baba yake ni Mgiriki. Walipokuwa wakienda walipita kwenye miji na kutoa maagizo kwa makanisa ili kuyatii maagizo hayo yaliandikwa na mitume na wazee huko Yerusalemu. Hivyo makanisa yakaimarishwa katika imani na walioamini wakaongezeka kwa idadi kila siku. Paulo na mwenzake wakaenda Firigia na Galatia, kwani Roho wa Mungu aliwakataza kuhubiri neno huko kwenye jimbo la Asia. Walipokaribia Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu akawakataza. Kwa hiyo wakapita Misia wakaja mpaka Mji wa Troa. Maono yalimtokea Paulo usiku, kulikuwa na mtu wa Makedonia amesimama, akimwita na kusema “Njoni mtusaidie huku Makedonia”. 10 Paulo alipoona maono, mara tukajiandaa kwenda Makedonia, akijua kwamba Mungu alituita kwenda kuwahubiria injili. 11 Hivyo tukaondoka kutoka Troa, tukaenda moja kwa moja Samothrake, na siku iliyofuata tukafika mji wa Neapoli. 12 Kutoka hapo tukaenda Filipi ambao ni moja ya mji wa Makedonia, mji muhimu katika wilaya na utawala wa Kirumi na tukakaa siku kadhaa. 13 Siku ya Sabato, tulikwenda nje ya lango kwa njia ya mto, sehemu ambayo tulidhania kutakuwa na mahali pa kufanyia maombi. Tulikaa chini na kuongea na akinamama waliokuja pamoja. 14 Mwanamke mmoja aitwaye Lidia, muuzaji wa zambarau, kutoka katika mji wa Tiatira, mwenye kumwabudu Mungu, alitusikiliza. Bwana alimfungua moyo wake na kuweka maanani maneno yaliyosemwa na Paulo. 15 Baada ya kubatizwa, yeye na nyumba yake yote, alitusihi akisema “ kama mmeniona kuwa mimi ni mwaminifu katika Bwana, basi nawasihi muingie na kukaa kwangu”. Akatusihi sana. 16 Ikawa kwamba, tulipokuwa tunaenda mahali pa kuomba, msichana mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi akakutana nasi. Alimletea bwana wake faida nyingi kwa kubashiri. 17 Mwanamke huyu alimfuata Paulo pamoja na sisi, akipiga kelele na kusema “Hawa wanaume ni watumishi wa Mungu aliye Mkuu, wanaowatangazia ninyi habari ya wokovu”. 18 Alifanya hivyo kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa amekasirishwa na tendo hilo, aligeuka nyuma na kumwambia pepo, “ Nakuamuru kwa Jina la Yesu umtoke ndani yake.” Naye akatoka na kumwacha mara moja. 19 Mabwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limeondoka, waliwakamata Paulo na Sila na kuwaburuza sokoni mbele ya wenye mamlaka. 20 Walipowafikisha kwa mahakimu, walisema, “Hawa wanaume ni Wayahudi na wanasababisha ghasia kubwa katika mji wetu. 21 Wanafundisha mambo ambayo siyo sheria sisi kuyapokea wala kuyafuata kama Warumi.” 22 Umati ukawainukia kinyume Paulo na Sila, mahakimu wakararua nguo zao na kuwavua na kuamuru wachapwe viboko 23 Baada ya kuwachapa viboko vingi, waliwatupa gerezani na kumuamuru askari wa gereza kuwalinda vyema. 24 Baada ya kupokea amri hiyo, askari wa gereza aliwatupa katika chumba cha ndani ya gereza na kuwafunga miguu yao kwenye sehemu alipowahifadhi. 25 Wakati wa usiku wa manane, Paulo na Sila wakawa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwasikiliza, 26 Ghafla kukatokea tetemeko kuu na misingi ya gereza ikatikiswa, milango ya gereza ikafunguka, na minyororo ya wafungwa wote ikalegezwa. 27 Mlinzi wa Gereza aliamka kutoka usingizini na akaona milango yote ya gereza imefunguliwa; hivyo akachukua upanga wake maana alitaka kujiua kwa sababu alifikiri wafungwa wote walikwishatoroka, 28 Lakini, Paulo akapiga kelele kwa sauti kuu, akisema “usijidhuru kwa sababu wote tuko mahali hapa”. 29 Mlinzi wa gereza aliomba taa ziletwe na akaingia ndani ya gereza kwa haraka, akitetemeka na kuogopa, akawaangukia Paulo na Sila, 30 na kuwatoa nje ya gereza na kusema, “Waheshimiwa, nifanye nini ili nipate kuokoka?” 31 Nao wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.” 32 Walinena neno la Bwana kwake, pamoja na watu wote wa nyumbani kwake, 33 Mlinzi wa gereza aliwachukua usiku ule na kuwaosha sehemu walizoumia, yeye pamoja na watu wa nyumbani mwake wakabatizwa mara. 34 Akawaleta Paulo na Sila nyumbani kwake na kuwatengea chakula. Naye akawa na furaha kuu pamoja na watu wa nyumbani mwake kwa sababu walimwamini Mungu. 35 Ilipokuwa mchana, mahakimu walituma ujumbe kwa yule mlinzi wa gereza wakisema, “Waruhusu wale watu waende”, 36 Mlinzi wa gereza akamjulisha Paulo juu ya maneno hayo ya kuwa, “Mahakimu walituma ujumbe niruhusu mwondoke: hivyo tokeni nje na mwende kwa amani.” 37 Lakini Paulo akawaambia, “Walitupiga hadharani, watu ambao ni Warumi bila kutuhukumu na waliamua kututupa gerezani; halafu sasa wanataka kututoa kwa siri? Hapana, haitawezekana, wao wenyewe waje kututoa mahali hapa”. 38 Walinzi wakawajulisha mahakimu juu ya maneno hayo, mahakimu wakaogopa sana pale walipojua kuwa Paulo na Sila ni Warumi. 39 Mahakimu wakaja na kuwasihi watoke, na walipowatoa nje ya gereza, waliwaomba Paulo na Sila watoke nje ya mji wao. 40 Kwa hiyo Paulo na Sila wakatoka nje ya gereza wakaja nyumbani kwa Lidia. Paulo na Sila walipowaona ndugu, waliwatia moyo na kisha kuondoka katika mji huo.