7
Kuhani mkuu akasema,”mambo haya ni ya kweli”? Stephano akasema, “Ndugu na mababa zangu, nisikilizeni mimi: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu wakati alipokuwa Mesopotamia, kabla hajaishi Harani,' akamwambia,' Ondoka katika nchi yako na jamaa zako na uende katika nchi nitakayokuonyesha'. Kisha akaondoka katika nchi ya Ukaldayo akaishi Harani, kutoka hapo, baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta kwenye nchi hii, wanayoishi sasa. Hakumpa chochote kama urithi wake, hapakuwa na sehemu hata ya kuweka mguu. Lakini Abrahamu aliahidiwa hata kabla hajapata mtoto kuwa atapewa nchi kama miliki yake na uzao wake. Mungu alinena naye hivi, ya kwamba wazao wake wangeishi katika nchi ya ugeni, na kwamba wenyeji wa huko watawafanya kuwa watumwa wao na kuwatenda vibaya kwa muda wa miaka mia nne. Na Mungu akasema, nitalihukumu taifa ambalo litawafanya mateka, na baada ya hapo watatoka na kuniabudu katika sehemu hii.' Na akampa Abrahamu agano la tohara, hivyo Abrahamu akawa baba wa Isaka akamtahiri siku ya nane; Isaka akawa baba wa Yakobo, na Yakobo akawa baba wa mababu zetu kumi na wawili. Mababu zetu wakamwonea wivu Yusufu wakamuuza katika nchi ya Misri, na Mungu alikuwa pamoja naye, 10 na akamwokoa katika mateso yake, na akampa fadhili na hekima mbele ya Farao mfalme wa Misri. Farao akamfanya awe mtawala juu ya Misri na juu ya nyumba yake yote. 11 Basi kukawa na njaa kuu na mateso mengi katika nchi ya Misri na Kanani, na baba zetu hawakupata chakula. 12 Lakini Yakobo aliposikia kuna nafaka Misri, aliwatuma baba zetu kwa mara ya kwanza. 13 Katika safari ya pili Yusufu akajionyesha kwa ndugu zake, familia ya Yusufu ikajulikana kwa Farao. 14 Yusufu akawatuma ndugu zake kwenda kumwambia Yakobo baba yao aje Misri, pamoja na jamaa yake, jumla ya watu wote ni sabini na tano. 15 Hivyo Yakobo akashuka Misri; kisha akafa yeye pamoja na baba zetu. 16 Wakachukuliwa hata Shekemu wakazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alilinunua kwa vipande vya fedha kutoka kwa wana wa Hamori huko Shekemu. 17 Wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimwahidi Abrahamu ulipokaribia, watu wakiwa wameongezeka huko Misri, 18 wakati huo aliinuka mfalme mwingine juu ya Misri, mfalme asiyejua kuhusu Yusufu. 19 Huyo mfalme mwingine akawadanganya watu wetu na kuwatenda mabaya baba zetu, na kuwatupa watoto wao wachanga ili wasiishi. 20 Katika kipindi kile Musa alizaliwa; alikuwa mzuri mbele za Mungu, akalelewa miezi mitatu katika nyumba ya baba yake. 21 Wakati alipotupwa, binti wa Farao alimchukua akamlea kama mwanaye. 22 Musa alifundishwa mafundisho yote ya Kimisri; alikuwa na nguvu katika maneno na matendo. 23 Lakini baada ya kutimiza miaka arobaini, ikamjia katika moyo wake kuwatembelea ndugu zake, wana wa Israeli. 24 Alipomwona Mwisraeli akitendewa mabaya, Musa alimtetea na kulipiza kisasi aliyekuwa akimwonea kwa kumpiga Mmisiri: 25 akifikiri kuwa ndugu zake watafahamu kwamba Mungu anawaokoa kwa mkono wake, lakini hawakufahamu. 26 Siku iliyofuata akaenda kwa baadhi ya Waisraeli waliokuwa wanagombana; akajaribu kuwapatanisha; akisema,' Mabwana, Ninyi ni ndugu; mbona mnakoseana ninyi kwa ninyi,? 27 Lakini aliyemkosea jirani yake akamsukumia mbali, na kusema, 'Nani kakufanya mtawala na muhukumu wetu? 28 Wewe unataka kuniua, kama ulivyomuua Mmisri jana?” 29 Musa akakimbia baada ya kusikia hivyo; akawa mgeni katika nchi ya Midiani, ambapo akawa baba wa wana wawili. 30 Baada ya miaka arobaini kupita, malaika akamtokea katika jangwa la mlima Sinai, katika mwali wa moto ndani ya kichaka. 31 Wakati Musa alipoona moto, alishangaa na kustaajabia kile alichokiona, na alipojaribu kukisogelea ili kukitazama, sauti ya Bwana ikamjia Ikisema, 32 'Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Yakobo'. Musa alitetemeka na hakuthubutu kuangalia. 33 Bwana akamwambia, 'Vua viatu vyako, sehemu uliposimama ni mahali patakatifu. 34 Nimeona mateso ya watu wangu waliopo Misri; Nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka ili niwaokoe; sasa njoo, nitakutuma wewe Misri.' 35 Huyu Musa ambaye waliyemkataa, wakati waliposema, 'nani kakufanya kuwa mtawala na mwamuzi wetu?'_ alikuwa ndiye ambaye Mungu alimtuma awe mtawala na mkombozi. Mungu alimtuma kwa mkono wa malaika ambaye alimtokea Musa kichakani. 36 Musa aliwaongoza kutoka Misri baada ya kufanya miujiza na ishara katika Misri na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa kwa kipindi cha miaka arobaini. 37 Ni Musa huyu ndiye aliyewambia watu wa Isiraeli kuwa, 'Mungu atawainulieni nabii kutoka miongoni mwa ndugu zenu, nabii kama mimi'. 38 Huyu ni mtu ambaye alikuwa katika mkutano jangwani na malaika ambaye aliongea naye katika mlima Sinai. Huyu ndiye mtu ambaye alikuwa na baba zetu, huyu ni mtu ambaye alipokea neno lililo hai na kutupatia sisi. 39 Huyu ni mtu ambaye baba zetu walikataa kumtii; walimsukumia mbali, na katika mioyo yao waligeukia Misri. 40 Katika kipindi hicho walimwambia Haruni.'tutengenezee miungu itakayotuongoza. Huyo Musa, aliyekuwa akituongoza kutoka katika nchi ya Misri, hatujui kilichompata.' 41 Hivyo wakatengeneza ndama kwa siku hizo na wakatoa sadaka kwa hiyo sananmu na wakafurahi kwa sababu ya kazi ya mikono yao. 42 Lakini Mungu aliwageuza na kuwapa waabudu nyota wa angani, kama ilivyoandikwa kwenye kitabu cha manabii, 'Je Mmenitolea mimi sadaka za wanyama mliowachinja jangwani kwa muda wa miaka arobaini, nyumba ya Israeli? 43 Mmekubali hema ya kukutania ya Moleki na nyota ya mungu refani, na picha mliyoitengeneza na kuwaabudu wao: na nitawapeleka mbali zaidi ya Babeli.' 44 Baba zetu walikuwa na hema ya kukutania ya ushuhuda jangwani, kama Mungu alivyoamuru alipoongea na Musa, kwamba angeitengeneza kwa mfano wa ule aliouona. 45 Hili ni hema ambalo baba zetu, kwa wakati wao, waliletwa katika nchi na Joshua. Hii ilitokea wakati walipoingia kumiliki taifa ambalo Mungu aliwafukuza kabla ya uwepo wa baba zetu. Hii ilikuwa hivi hadi siku za Daudi, 46 ambaye alipata kibali machoni pa Mungu,' na akaomba kutafuta makao kwa Mungu wa Yakobo. 47 Lakini Selemani alimjengea nyumba ya Mungu. 48 Hata hivyo Aliye Juu haishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono; hii ni kama nabii alivyosema, 49 Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni sehemu ya kuwekea miguu yangu. Nyumba ya aina gani mtanijengea?, asema Bwana: au ni wapi sehemu yangu ya kupumzikia? 50 Siyo mkono wangu uliofanya hivi vitu vyote?' 51 Enyi watu wenye shingo ngumu msiotahiriwa mioyo na masikio, kila mara mnampinga Roho Mtakatifu,' mnatenda kama baba zenu walivyotenda. 52 Ni nabii gani katika manabii ambaye baba zenu hawakumtesa?. Waliwaua manabii wote waliotokea kabla ya ujio wa Mmoja mwenye Haki,'na sasa mmekuwa wasaliti na wauaji wake pia, 53 enyi watu mliopokea sheria ile iliyoagizwa na malaika lakini hamkuishika.” 54 Kisha wajumbe wa baraza waliposikia mambo haya, walichomwa mioyo yao, wakamsagia meno Stefano. 55 Lakini yeye, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama mbinguni kwa makini na akauona utukufu wa Mungu,' na kumwona Yesu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Angalia nimeona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adam amesimama mkono wa kuume wa Mungu.” 57 Lakini wajumbe wa baraza wakapiga kelele kwa sauti za juu, wakaziba masikio yao, wakamkimbilia kwa pamoja, 58 wakamtupa nje ya mji na wakampiga mawe: na mashahidi wakavua nguo zao za nje na kuweka chini karibu na miguu ya kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wakimpiga mawe Stefano, aliendelea kumwita Bwana na kusema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu,”. 60 Akapiga magoti na kuita kwa sauti kubwa, “Bwana, usiwahesabie dhambi hii. “Aliposema haya, akakata roho.