10
1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ujumbe ulifunuliwa kwa Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza. Ujumbe huu ulikuwa ni wa kwelil. Ulihusu vita kuu. Danieli aliufahamu ujumbe alipopata ufumbuzi kutoka katika maono.
2 Katika siku hizo, mimi Danieli, nilikuwa katika maombolezo kwa wiki tatu.
3 Sikula chakula kizuri, sikula nyama, sikunywa divai, na sikujipaka mafuta mwenyewe mpaka ukamilifu wa wiki tatu nzima.
4 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa niko karibu na mto mkubwa (ambao ni Tigrisi),
5 Nilitazama juu na nikamwona mtu aliyevaa kitani, akiwa na mkanda kiunoni mwake uliotengenezwa kwa dhahabu safi kutoka Ufazi.
6 Mwili wake ulikuwa kama kito, na sura yake ilikuwa kama radi. Macho yake yalikuwa kama miali ya tochi, na mikono yake na miguu yake ilikuwa kama shaba iliyosafishwa. Sauti ya maneno yake ilikuwa kama sauti ya umati mkubwa wa watu.
7 Mimi, Danieli peke yangu niliyaona maono, na watu niliokuwa na pamoja hawakuyaona maono. Lakini, jambo kuu la kuogofya liliwaijia juu yao, na walikimbia na kujificha wao wenyewe.
8 Hivyo niliachwa peke yangu na niliyaona maono haya ajabu. Hakuna nguvu iliyobakia ndani yangu; mwonekano wangu wa kung'aa ulibadilika na kuwa mwonekano wa uharibifu, na hazikubakia nguvu ndani yangu.
9 Kisha nikasikia maneno yake, na nilipoyasikia, nilianguka kifudifudi na kupata usingizi mzito.
10 Mkono ulinigusa, na ilinifanya nitetemeke katika magoti yangu na viganja vya mikono yangu.
11 Malaika aliniambia, “Danieli, mtu aliyetunzwa sana, yafahamu maneno ninayokwambia wewe. Simama wima, kwa kuwa nimeshakutuma.” Na alipomaliza kuniambia ujumbe huu, nilisimama nikiwa natetemeka.
12 Kisha aliniambia, “Usiogope, Danieli. Tangu siku ya kwanza ulipoiweka akili yako kutaka kufahamu na kujinyenyekeza mwenyewe mbele ya Mungu, maneno yako yalisikiwa, na nimekuja kwasababu ya maneno yako.
13 Mwana wa mfalme wa ufalme wa Uajemi alinizuia, na niliwekwa huko na mfalme wa Uajemi kwa siku ishirini na moja. Lakini Mikaeli, mmoja kati ya wakuu alikuja kunisaidia.
14 Sasa nimekuja kukusaidia ili ufahamu kile kitakachotokea kwa watu wako katika siku za mwisho. Kwa kuwa maono ni kwa ajili siku ambazo hazijatokea bado.
15 Na alipokuwa akali akiniambia maneno haya, niligeuza uso wangu na kuuelekeza chini na sikuwa na uwezo wa kuzungumza.
16 Yeye aliyekuwa kama wana wa mtu alinigusa mdomo wangu na nifumbua kinywa changu na nilimwambia huyo aliyekuwa amesimam mbele yangu: “Bwana wangu, niko katika masumbuko makali kwasababu ya maono; sina nguvu ndani yangu iliyosalia.
17 Mimi ni mtumishi wako. Je ninawezaje kuongea na Bwana wangu? Kwa kuwa sasa sina nguvu, na hakuna pumzi iliyosalia ndani yangu.”
18 Tena yule mwenye mwonekano wa mtu alinigusa na kunitia nguvu.
19 Alisema, “Usiogope, mtu ulithaminiwa sana. Amani na iwe kwako! Uwe mwenye nguvu, uwe na nguvu!” Na alipokuwa anaongea na mimi, nilipata nguvu. Nilimwambia, “Bwana wangu na aseme, kwa kuwa umenitia nguvu.”
20 Aliniambia, “Je unajua ni kwanini nimekuja kwako? Nitarudi hivi karibuni kupigana na mkuu wa Uajemi. Na nitakapoenda, mkuu wa Ugiriki atakuja.
21 Lakini nitakwambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Ukweli. Hakuna yeyote anayejionesha kuwa na nguvu pamoja nami dhidi yao, isipokuwa Mikaeli mkuu wenu.”