9
1 Dario mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi. Alikuwa na Ahasuero ambaye alifanywa mfalme juu ya ufalme wa watu wa Babeli.
2 Sasa katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario, mimi Danieli, nilikuwa najisomea vitabu vilivyo na neno la Yahweh, neno ambalo lilikuwa limemjia Yeremia nabii. Niligundua kwamba kungekuwa na miaka sabini hadi mwisho wa kuachwa kwa Yerusalemu ungefika.
3 Niliugeuza uso wangu kumwelekea Bwana Mungu, ili kumtafuta yeye kwa sala na maombi, kwa kufunga, na kuvaa nguo za magunia na kukaa katika majivu.
4 Nilimwomba Yahweh Mungu wangu, na niliungama dhambi zetu. Nilisema, “Tafadhali, Bwana, wewe ni Mungu mkuu na mwenye kuheshimiwa, wewe hutunza maagano na uliye mwaminifu katika kuwapenda wale wanaokupenda wewe na kuzishika amri zako.
5 Tumetenda dhambi na tumefanya yaliyo mabaya. Tumeenenda kwa uovu na tumeasi, tumegeuka upande kinyume na amri na maagizo yako.
6 Hatujawasikiliza watumishi wako manabii walizungumza na wafalme wetu, viongozi wetu, baba zetu, na kwa watu wote wa nchi kwa jina lako.
7 Kwako Bwana, kuna uadilifu. Hata hivyo, kwetu kuna aibu katika nyuso zetu, kwa watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalem, na kwa Israeli yote. Hii ni pamoja na wale walio karibu na wale walio mbali katika nchi zote ambazo kwazo uliwatawanya. Hii ni kwasababu ya udanganyifu mkubwa tulioufanya kinyume chako.
8 Kwetu sisi, Yahweh, kuna fedheha katika nyuso, na kwa wafalme wetu, na kwa viongozi wetu, na kwa baba zetu, kwasababu tumekutenda dhambi wewe.
9 Kwa Bwana Mungu wetu kuna huruma na msamaha, kwa kuwa tumemwasi yeye.
10 Hatujaitii sauti ya Yahweh Mungu wetu kwa kutembea katika sheria zake alizotupatia kupitia watumishi wake manabii.
11 Israeli wote wameiasi sheria yako na kugeukia upande, kwa kukataa kuitii sauti yako. Laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu, zimemwagwa juu yetu kwa kuwa tummetenda dhambi.
12 Yahweh ameyathibitisha maneno ambayo aliyasema kinyume na sisi na kinyume na viongozi wetu juu yetu, kwa kuleta juu yetu janga kubwa. Kwa kuwa chini ya mbingu yote haijawahi kufanyika kitu chochote ambacho kinaweza kulinganishwa na kile kilichofanyika huko Yerusalemu.
13 Kama ilivyoandikwa kwenye sheria ya Musa, baa hili lote limetupata, ingawa bado hatujaomba rehema kutoka kwa Yahweh Mungu wetu kwa kugeuka na kuacha maovu yetu na kuufuata ukweli wako.
14 Hivyo basi, Yahweh ameyaweka tayari maafa na ameyaleta juu yetu, kwa kuwa Yahweh Mungu wetu ni mwenye haki katika matendo yote anayoyafanya, ingawa bado hatujaitii sauti yake.
15 Basi sasa, Bwana Mungu wetu, uliwatoa watu wako katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu, na umejifanyia jina maarufu kwa ajli yako mwenyewe, hata siku hii ya leo. Lakini bado tumekutenda dhambi; tumefanya mambo ya hila. Kwasababu ya matendo yako yote ya haki,
16 Bwana, iache hasira na ghadhabu yako iwe mbali na mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Hii ni kwasababu ya dhambi zetu, na kwasababu ya uovu wa baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamekuwa kitu cha kudharauliwa na wote wanaotuzunguka.
17 Basi sasa, Mungu wetu, sikiliza sala za mtumishi wako na maombi yake kwa ajili ya rehema; kwa ajili yako, Bwana ufanye uso wako ung'ae katika sehemu yako takatifu iliyoachwa ukiwa.
18 Mungu wangu, fungua masikio yako na usikie; fumbua macho yako na uone. Tumeharibiwa; utazame mji unaoitwa kwa jina lako. Hatukuombi msaada wako kwasababu ya haki yetu, ila kwasababu ya rehema zako kuu.
19 Bwana, sikiliza! Bwana, samehe! Bwana, tuangalie na ufanye jambo! Kwa ajili yako mwenyewe, usichelewe, Mungu wangu, kwa kuwa mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.”
20 Nilipokuwa ninaongea kwa kuomba na kuungama dhambi yangu na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuwasilisha maombi yangu mbele ya Yahweh Mungu wangu kwa niaba ya mlima mtakatifu wa Mungu.
21 Nilipokuwa ninaomba, mtu Gabrieli, ambaye nilikuwa nimemwona katika ndoto hapo awali, alipaa kwa kasi kushuka kuja nilipo, ilikuwa ni wakati wa sadaka ya jioni.
22 Alinipa ufahamu na aliniambia, “Danieli, nimekuja sasa ili nikupe utambuzi na ufahamu.
23 Ulipoanza kuomba rehema, amri ilitolewa na nimekuja kukueleza jibu, kwa kuwa unapendwa sana. Hivyo basi, tafakari neno hili na uufahamu ufunuo.
24 Miaka sabini na saba zimeamriwa kwa ajili ya watu wako na mji wako mtakatifu kukomesha hatia na kumaliza dhambi, na kuleta haki ya milele, na kutimiza maono na unabii, na kupaweka wakfu mahali patakatifu sana.
25 Ujue na kufahamu kuwa tangu kupitishwa kwa amri ya kurudi na kuijenga upya Yerusalemu mpaka ujio wa mpakwa mafuta (atakayekuwa kiongozi), kutakuwa na majuma saba na majuma sitini na mbili. Yerusalemu itajengwa pamoja na mitaa yake na handaki, licha ya kuwepo kwa nyakati za shida
26 Baada ya miaka ya majuma sitini na mbili, mtiwa mafuta ataharibiwa na atakuwa hana kitu chochote. Jeshi la kiongozi ajaye litauangamiza mji na mahali patakatifu. Mwisho wake utatatokea kwa gharika, na kutakuwa na vita hata mwisho. Uharibifu umekwisha amriwa.
27 Atalithibitisha agano pamoja na watu wengi kwa miaka saba. Katikati ya miaka saba atakomesha dhabihu na sadaka. Baada ya chukizo la uharibifu atatokea mtu atakayeleta ukiwa. Mwisho kamili na uharibifu umeamriwa kutokea kwa yeye aliyesababisha ukiwa.”