27
Katika mwanzo wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hil lilimjia Yeremia kutoka kwa Yahwe. (Ingawa nakala nyingi za Kiebrania zinasema “Yehoyakimu, matoleo mengi ya kisasa yanasema “Sedekia”, kwa sababu tukio katika sura hii lilitokea katika kipindi cha utawala wake). Hiki ndicho Yahwe alisema kwangu, “Tengeneza vifungo na nira kwa ajili yako mwenyewe. Ziweke shingoni mwako. Kisha akawatuma kwenda kw mfalme wa Edomu, mfalme wa Moabu, mfalme wa watu wa amoni, mfalme wa Tiro, na kwa mfalme wa Sidoni. Watume kwa mkono wa wajumbe hao wa wafalme ambao walikuja Yerusalemu kwa Sedekia mfalme wa Yuda. Toa amri kwao kwa ajili ya mabwana zao na sema, ' Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Hivyo ndivyo utakavyosema kwa mabwana zenu, Mimi mwenyewe niliiumba dunia kwa nguvu zangu kuu na mkono wangu ulioinuka. Pia niliwaumba watu na wanyama juu ya dunia, na nikawatoa kwa yeyote aliyesahihi katika macho yangu. Kwa hiyo sasa, Mimi mwenyewe naziweka nchi hizi zote kwenye mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu. Pia, ninavikabidhi kwake viumbe hai vyote katika mashamba ili vimtumikie. Kwa maana mataifa yote watamtumikia yeye, wanaye, na wajukuu zake hadi muda wa nchi yake ufike. Kisha mataifa mengi na wafalme wengi watamtiisha. Kwa hiyo taifa na ufalme ambo haumtumikii Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na ule usioweka shingo yake chini ya nira ya Nebukadreza mfalme wa Babeli—nitaliadhibu taifa hilo kwa upanga, njaa, na pigo—hili ni tangazo la Yahwe—hadi nitakapokuwa nimewateketeza kwa mkono wake. Kwa hiyo msiwasikilize manabii wenu, wabashiri wenu, waonaji wenu, ndoto zenu, watambuzi wenu, ambao wamekuw wakisema kwenu na kusema, ' Msimtumikie mfalme wa Babeli.' 10 Kwa maana wanatabiri uongo kwenu ili kuwapeleka mbali na nchi zenu, kwa maana nitawapeleka mbali, na mtakufa. 11 Lakini taifa ambalo wataweka shingo zao chini ya nira ya mfalme wa Babeli na kumtumikia, nitawaruhusu kupumzika katika nchi yao—hili ni tangazo la Yahwe—na watailima na kufanya nyumba zao humo.”” 12 Kwa hiyo nilisema kwa Sedekia mfalme wa Yuda na kumpa ujumbe huu, “Ziwekeni shingo zenu chini ya nira ya mfalme wa Babeli na mtumikieni yeye na watu wake, na mtaishi. 13 Kwa nini mfe—wewe na watu wako—kwa upanga, njaa, na pigo, kama vile nilivyotangaza kuhusu taifa ambalo watapuuza kumtumikia mfalme wa Babeli? 14 Msisikilize maneno ya manabii wanaozungumza kwenu na kusema, 'Msimtumikie mfalme wa Babeli', kwa maana wanatabiri uongo kwenu. 15 'Kwa maana mimi sikuwatuma—hili ni tangazo la Yahwe—kwa maana wanatabiri uongo katika jina langu ili kwamba niwafukeze inje na muangamie, ninyi nyote na manabii wanaotabiri kwenu.”' 16 Nilitangaza hili kwa makuhani na watu wote na kusema, “Yahwe anasema hivi: Msisikilize maneno ya manabii wanaotabiri kwenu na kusema, 'Angalia! Vyombo vya nyumba ya Yahwe vinarudishwa kutoka Babeli sasa hivi!' Wanatabiri uongo kwenu. 17 Msiwasikilize. Mtamtumikia mfalme wa Babeli na mtaishi. Kwa nini mji huu uangamizwe? 18 Kama ni manabii, na kama neno la Mungu limekuja kwao kweli, basi wamwombe Yahwe wa majeshi asivipeleke Babeli vyombo vilivyosalia katika nyumba, nyumba ya mfalme wa Yuda, na Yerusalemu. 19 Yahwe wa majeshi anasema hivi kuhusu zile nguzo, bahari, na kitako, na vyombo vyote vilivyosalia katika mji huu— 20 vyombo ambavyo Nebukadreza mfalme wa Babeli hakuvichukua wakati alipomchukua Yekonia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika utumwa kutoka Yerusalemu kwenda Babeli pamoja na wakuu wote wa Yuda na Yerusalemu. 21 Yahwe wa majeshsi, Mungu wa Israeli, anasema hivi kuhusu vyombo vilivyosalia katika nyumba ya Yahwe, nyumba ya mfalme wa Yuda, na Yerusalemu, 22 'Vitaletwa Babeli, na vitabaki huko hadi siku niyovipangia kutimia—hili ni tangazo la Yahwe—kisha nitavileta na kuvirudisha kataika sehemu hii.”