10
Ikawa Adonizedeki, mfalme wa Yerusalemu, alisikia kuwa Yoshua ameiteka Ai na ameiteketeza kabisa, kama alivyokwisha kufaya huko Yeriko na mfalme wake. Na alisikia jinsi ambavyo watu wa Gibeoni walivyofanya amani na watu wa Israeli na walikuwa wanaishi miongoni mwao. Watu wa Yerusalemu waliogopa sana kwasababu Gibeoni ulikuwa mji mkubwa, kama mmoja wa miji ya kifalme. Ilikuwa kubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa ni mashujaa wenye nguvu. Hivyo Adonizedeki, mfalme wa Yerusalemu, alituma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarimuthi, na kwaYafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Eguloni: “Njooni kwangu na mnisaidie. Tuishambulie Gibeoni kwasababu wamefanya amani na Yoshua pamoja na watu wa Israeli. Wafalme watano wa Waamori; mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarimuthi, mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Eguloni walikwea, wao pamoja na majeshi yao yote. Walipanga sehemu yao kinyume na Wagibeoni na waliwashambulia. Watu wa Gibeoni walituma ujumbe kwa Yoshua na kwa jeshi huko Giligali. Walisema, “ Upesi! Msiuondoa mkono wenu kutoka kwa watumishi wenu. Kwaeni mje haraka na mtuokoe. Mtusaide, maana wafalme wote wa Waamori wanaoishi katika nchi ya milima wamekusanyika kwa pamoja ili watushambulie. “Yoshua alipanda kutoka Giligali, yeye na watu wote wa vita pamoja naye, na watu wote wapiganaji. Yahweh akamwambia Yoshua, “Usiwaogope. Nimewatiwa wote katika mkono wako. Hakuna hata mmoja wao atakayeweza kuzuia mashambulizi yako.” Baada ya kutembea usiku kucha kutoka Giligali, ghafla Yoshua aliwafikilia. 10 Na Yahweh alichanganya maadui mbele za Israeli - ambao waliwaua mauaji makubwa mno huko Gibeoni, na wale waliowafuata njiani iendayo Bethi Horoni, nao waliuwaua katika njia iendayo Azeka na Makeda. 11 Na walipokuwa wakikimbia mbio kutoka kwa Waisraeli, chini ya mlima kutoka Bethi Horoni, Yahweh alitupa mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao wote katika njia iendayo Azeka, nao wakafa. Watu waliouawa kwa mawe walikuwa ni wengi zaidi kuliko wale waliouawa kwa upanga wa watu wa Israeli. 12 Kisha Yoshua akamwambia Yahweh katika siku ambayo Yahweh aliwapa watu wa Israeli ushindi dhidi ya Waamori. Hiki ndicho Yoshua alichosema kwa Yahweh mbele ya Israeli. “ Jua lisimame katika Gibeoni, na mwezi, usimame katika bonde la Aijaloni.” 13 Jua lilisimama, na mwezi ukaacha kwenda mpaka taifa lilipolipiza kisasi dhidi ya maadui zao. Je hili halikuandikwa katika Kitabu cha Yashari? Jua lilikaa katikati ya anga; halilkuzama kwa siku nzima hivi. 14 Haijawahi kutokea siku nyingine kama hiyo kabla au baada yake, wakati Yahweh alipotii sauti ya mtu. Kwa kuwa Yahweh alikuwa akifanya vita badala ya Israeli. 15 Yoshua na Israeli yote pamoja naye walirudi kambini huko Giligali. 16 Basi wale wafalme watano walikuwa wametoroka na kujificha wao wenyewe katika pango huko Makeda. 17 Taarifa zilimfikia Yoshua kusema, “Wafalme watano wamepatikana wamejificha katika pango huko Makeda!” 18 Yoshua akasema, “Viringisheni mawe makubwa katika mlango wa pango na muweke wanajeshi hapo ili kuwalinda. 19 Msibaki na kukaa nyie wenyewe. Bali wafuatilieni maadui zenu na kuwashumbulia kutokea kwa nyuma. Msiwaruhusu kuingia katika miji yao, kwa kuwa Yahweh Mungu wenu amewatia katika mkono wenu.” 20 Yoshua na wana Waisraeli walikuwa wamemaliza kuwaua kwa mauaji makubwa sana, mpaka pale walipokuwa wameteketezwa kabisa; watu wachache tu walipona waliotoroka walifika miji ya ngome. 21 Kisha jeshi lote lilirudi kwa Yoshua likiwa na amani katika kambi huko Makeda. Na hakuna hata mmoja aliyethubutu kusema hata neno moja kinyume na watu wa Israeli. 22 Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango, watoeni nje na waleteni kwangu hawa wafalme watano.” 23 Walifanya kama Yoshua alivyosema. Waliwaleta wafalme watano kutoka katika pango - mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni. 24 Na walipowaleta wafalme kwa Yoshua, alimwita kila mtu wa Israeli, na aliwaambia maakida wa wanajeshi waliokuwa wameenda vitani pamoja naye “ Kanyageni miguu yenu juu ya shingo zao.” Basi walikuja na kukanyaga miguu yao juu ya shingo zao. 25 Kisha akawaambia, 'Msiogope wala kufadhaika. uwe na moyo mkuu na jasiri. Na hiki ndicho Mungu atakachokifanya kwa maadui wenu wote ambao mtapigana nao'. 26 Kisha Yoshua akawashambulia na kuwaua wafalme. Aliwatundika wote watano juu ya miti. Waliwatundika juu ya miti hata jioni. 27 Ilipokuwa jioni, Yoshua alitoa maagizo, nao waliwashusha chini ya miti na kisha wakawatupa katika pango ambalo walikuwa wamejificha wao wenyewe. Waliweka mawe makubwa juu ya mlango wa pango. Mawe hayo yapo pale hadi leo hii. 28 Na kwa namna hii, katika siku hiyo Yoshua aliuteka mji wa Makeda na aliwaua watu wote huko kwa upanga, pamoja na mfalme wake. Aliwateketeza wote kabisa pamoja na kila kiumbe hai kilichokuwa huko. Hakuna hata mmoja aliyesalia. Alichomfanyia mfalme wa Makeda ni sawa sawa na kile alichokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko. 29 Yoshua na Israeli wote waliipita Makeda na kufika Libna. Na huko waliingia katika vita dhidi ya Libna. 30 Yahweh pia aliitia katika mkono wa Israeli pamoja na mfalme wake. Yoshua alishambulia kila kiumbe hai ndani yake kwa upanga. Hakuacha hai hata mtu mmoja. Alichomfanyia mfalme ni sawa sawa na kile alichokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko. 31 Baadaye Yoshua na Israeli wote pamoja naye walipanda kutoka Libna na kwenda Lakishi. Alipiga kambi karibu yake na wakafanya vita dhidi yake. 32 Yahweh aliitia Lakishi katika mkono wa Israeli. Yoshua aliiteka katika siku ya pili. Alishambulia kwa upanga kilia kiumbe hai kilichokuwa ndani yake, kama vile aliyokuwa amefanya huko Libna. 33 Kisha Horamu, mfalme wa Gezeri alikwea ili kuisaida Lakishi. Yoshua alimshambulia yeye na jeshi lake mpaka pale ambapo hapakuwa na mtu hata mmoja aliyesalia. 34 Baada ya hapo, Yoshua na Israeli wote walitoka Lakishi na kwenda Egloni. Walipiga kambi karibu yake na kisha wakafanya vita dhidi yake, 35 na siku hiyo hiyo wakaiteka. Waliupiga kwa upanga na waliteketeza kila mtu ndani yake kama vile Yoshua alivyofanya huko Lakishi. 36 Kisha Joshua na Israeli wote wakatoka Egloni na kwenda Hebroni. Wakainua vita dhidi yake. 37 Waliuteka mji na kuwaua kwa upanga watu wote ndani yake pamoja na mfalme wake, kujumuisha na vijiji vyote vilivyoizunguka. Waliteketeza kabisa kila kiumbe hai ndani yake, hawakuacha hata mtu mmoja aliyesalia, ni sawa sawa na vile Yoshua alivyoitenda Egloni. Aliiteketeza kabisa, na kila kiumbe hai ndani yake. 38 Baada ya hapo, Yoshua alirudi pamoja na jeshi lote la Israeli pamoja naye, wakasafiri kwenda Debiri na kufanya vita dhidi yake. 39 Aliuteka mji na mfalme wake, pamoja na vijiji vyake vya jirani. Waliwaua wote kwa upanga na waliteketeza kila kiumbe hai ndani yake. Joshua hakuacha hata mmoja hai, kama alivyokuwa amefanya kwa Hebroni na mfalme wake, na kama alivyokuwa amefanya kwa Libna na mfalme wake. 40 Yoshua aliishinda nchi yote, nchi ya milima, Negevu, nchi, nchi ya tambarare na nchi ya miteremko. Hakuna hata mfalme moja aliyebaki hai kati ya wafalme wake wote. Kwa kweli aliteketeza kila kiumbe hai, kama ambavyo Yahweh, Mungu wa Israeli alivyomwaagiza. 41 Yoshua aliwaua kwa upanga kutoka Kadeshi Barnea hadi Gaza, na nchi yote ya Gosheni hata Gibeoni. 42 Yoshua aliwateka wafalme wote hawa na nchi zao kwa wakati mmoja, kwasababu Yahweh, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli. 43 Baada ya hayo Yoshua na Waisraeli wote pamoja naye, walirudi katika kambi huko Gilgali.