11
1 Basi ikawa aliposikia haya, Yabini, mfalme wa Hazori, alituma ujumbe kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu.
2 Alituma pia ujumbe kwa wafalme walikuwa katika mlima wa kaskazini mwa nchi, katika bonde la Mto Yordani kusini mwa Kinerethi, katika nchi za tambarare, na katika nchi za milima ya Dori kuelekea magharibi.
3 Pia, alituma ujumbe kwa Wakanaani walioko mashariki na magharibi, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wayebusi katika nchi za milima, na Wahivi karibu na Mlima Hermoni katika nchi ya Mizipa.
4 Maadui zao wote walitoka pamoja nao, wanajeshi wengi sana, hesabu yao ilikuwa kama mchanga wa pwani. Walikuwa na farasi wengi sana na magari.
5 Wafalme wote hawa walikutana katika muda waliokuwa wameupanga, na walipiga kambi katika maji ya Meromu ili kupigana vita na Israeli.
6 Yahweh akamwambia Yoshua, “Usiogope mbele zao, kwa kuwa muda kama huu kesho ninawatia hao kwa Waisraeli wakiwa wafu. Utaivunja vunja miguu ya farasi zao, na utayachoma moto magari yao.”
7 Yoshua na watu wote wa vita walitoka na mara wakafika katika maji ya Meromu, na wakawashambulia maadui.
8 Yahweh akawatia maadui katika mkono wa Israeli, na waliwapiga kwa upanga na wakawafuata mpaka Sidoni, Misrefothi - Maimu, na katika bonde la Mizipa upande wa mashariki. Waliwaua wote hakuna hata mmoja aliyeachwa hai.
9 Yoshua aliwatendea kama vile Yahweh alivyomwambia. Alivunja miguu ya farasi na magari aliyachoma moto.
10 Kwa wakati huo, Yoshua alirudi na akauteka mji wa Hazori. Alimwua mfalme wake kwa upanga (Hazori ulikuwa ni kichwa cha falme hizi zote).
11 Waliwapiga kwa upanga kila kiumbe chenye uhai kilichokuwa huko, na alivitenga ili viteketezwe, hivyo hapakuwa na kiumbe hai kilichoachwa hai. Na kisha aliuchoma moto Hazori.
12 Yoshua aliiteka miji yote ya wafalme hawa. Aliwateka pia wafalme wake wote na akawapiga wote kwa upanga. Aliwateketeza kabisa kwa upanga, kama Musa mtumishi wa Yahweh alivyoagiza.
13 Waisraeli hawakuchoma moto mji wowote miongoni mwa miji iliyojengwa juu ya vilima vya vifuasi vya udongo, isipokuwa Hazori, ndio mji pekee ambao Yoshua aliuchoma kwa moto.
14 Jeshi la Israeli lilichukua nyara kutoka katika miji pamoja na mifugo kwa ajili yao wenyewe. Waliua kila mtu kwa upanga hadi pale walipokufa wote. Hakuna kiumbe hai kilichoachwa hai.
15 Kama vile Yahweh alivyomwagiza mtumishi wake Musa, na kwa namna hiyo hiyo, Musa alivyomwagiza Yoshua. Na katika mambo yote ambayo Yahweh alimwamuru Musa kuyafanya, Yoshua hakuacha kufanya hata jambo moja.
16 Yoshua alitwaa nchi hiyo yote, nchi ya milima, Negevu yote, nchi yote ya Gosheni, nchi ya vilima vidogo, bonde la Mto Yordani, nchi ya milima ya Israeli, na nchi tambarare.
17 Kutoka Mlima Halaki karibu na Edomu, kuelekea kasikazini hadi Baali Gadi katika bonde karibu na Lebanoni chini ya Mlima Hermoni, aliwateka wafalme wake wote na kuwaua.
18 Yoshua alipigana vita na wafalme wote kwa muda mrefu.
19 Hakuna hata mji mmoja uliofanya amani na jeshi la Israeli isipokuwa Wahivi walioishi Gibeoni. Israeli ilitwaa miji yote iliyosalia katika vita.
20 Kwa kuwa alikuwa ni Yahweh ambaye alikuwa ameifanya kuwa migumu mioyo yao ili wapande na kufanya vita dhidi ya Israeli, ili kwamba aweze kuwaangamiza kabisa, na kutowaonesha huruma, kama alivyomwaagiza Musa.
21 Kisha Yoshua akaja kwa wakati ule na aliiangamiza Anakimu. Aliyafanya haya katika nchi ya milima, huko Hebroni, Debiri, Anabu, na katika nchi yote ya Yuda, na katika nchi yote ya milima ya Israeli. Yoshua aliwaangamiza kabisa pamoja na miji yao.
22 Hakuna hata mmoja wa watu wa Anakimu aliyeachwa katika nchi ya Israeli, isipokuwa huko Gaza, Gathi na Ashidodi.
23 Hivyo Yoshua aliiteka nchi yote, kama vile Yahweh alivyomwambia Musa. Yoshua aliwapa Israeli kama urithi, kila kabila lilipewa sehemu yake. Kisha nchi ikapumzika bila vita.