15
Asubuhi na mapema wakuu wa makuhani walikutana pamoja na wazee na waandishi na baraza zima la wazee. Kisha wakamfunga Yesu wakampeleka kwa Pilato. Pilato akamwuliza, “wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” “Akamjibu, “Wewe umesema hivyo.” Wakuu wa makuhani wakaeleza mashitaka mengi juu ya Yesu. Pilato akamwuliza tena, “Hujibu chochote? Huoni jinsi wanavyokushtaki kwa mambo mengi? Lakini Yesu hakumjibu Pilato, na hiyo ilimshangaza. Kwa kawaida wakati wa sikukuu humfungulia mfungwa mmoja, mfungwa waliyemwomba. Kulikuwapo wahalifu gerezani, miongoni mwa wauaji kati ya walioasi wanaotumikia makosa yao. Alikuwepo mtu mmoja aitwaye Baraba. Umati ulikuja kwa Pilato, na kumwomba afanye kama alivyofanya huko nyuma. Pilato akawajibu na kusema, “Mnataka niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?” 10 Kwa kuwa alijua ni kwa sababu ya wivu wakuu wa makuhani walimkamata Yesu na kumleta kwake. 11 Lakini wakuu wa makuhani walichochea umati kupiga kelele kwa sauti kwamba afunguliwe Baraba badala yake. 12 Pilato akawajibu tena na kusema, “Nimfanye nini Mfalme wa Wayahudi? 13 Wakapiga kelele tena, “Msulibishe!” 14 Pilato akasema, “Amefanya jambo gani baya?” Lakini wakazidi kupiga kelele zaidi na zaidi “Msulibishe.” 15 Pilato akitaka kuwaridhisha umati, akawafungulia Baraba. Akampiga Yesu mijeledi kisha akamtoa ili asulibiwe. 16 Askari walimwongoza hadi ndani ya ua (ule ulio ndani ya kambi) na walikusanyika pamoja kikosi cha askari. 17 Wakamvika Yesu kanzu ya rangi ya zambarau, na wakasokota taji ya miiba wakamvika. 18 Wakaanza kumdhihaki na kusema, “Salam, Mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga kichwani kwa mwanzi na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake kwa kumheshimu. 20 Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua ile kanzu ya rangi ya zambarau na kumvika mavazi yake, na wakamtoa nje kwenda kumsulibisha. 21 Wakamlazimisha mpita njia kumsaidia, aliyekuwa anaingia mjini kutoka shamba. Aitwaye Simoni Mkirene (baba yake Iskanda na Rufo); wakamlazimisha kubeba msalaba wa Yesu. 22 Askari wakampeleka Yesu mahali paitwapo Goligotha (maana ya tafsiri hii ni, Sehemu ya Fuvu la kichwa). 23 Wakampa mvinyo iliyochanganywa na manemane, lakini hakunywa. 24 Wakamsulibisha na wakagawana mavazi yake, wakayapigia kura kuamua kipande atakachopata kila askari. 25 Yapata saa tatu asubuhi walipomsulibisha. 26 Wakaweka juu yake ubao ulioandikwa shitaka, “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Walimsubisha pamoja na majambazi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine kushoto kwake. 28 (Zingatia: Mstari huu, “Na maandiko yakatimia yaliyonena” haumo katika nakala za kale). 29 Nao waliokuwa wakipita walimtukana, wakitikisa vichwa vyao wakisema, “Aha! wewe utakayevunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30 jiokoe mwenyewe na ushuke chini toka msalabani!” 31 Kwa namna ile ile wakuu wa makuhani walimdhihaki wakisemezana, pamoja na waandishi na kusema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe. 32 Kristo Mfalme wa Israel, shuka chini sasa toka msalabani, ili tuweze kuona na kuamini.” Na wale waliosulubiwa pamoja naye pia walimdhihaki. 33 Ilipofika saa sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa tisa. 34 Wakati wa saa tisa, Yesu alipiga kelele kwa sauti kubwa, “Eloi, Eloi, lama sabaktani?” ikiwa na maana “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” 35 Baadhi ya hao waliosimama waliposikia wakasema, “Tazama, anamwita Eliya.” 36 Mtu mmoja akakimbia, akajaza siki katika sponji na kuiweka juu ya mti wa mwanzi, akampa ili anywe. Mtu mmoja akasema, “Ngoja tuone kama Eliya atakuja kumshusha chini.” 37 Kisha Yesu akalia kwa sauti kubwa na akafa. 38 Pazia la hekalu likagawanyika vipande viwili toka juu mpaka chini. 39 Ofisa mmoja aliyekuwa amesimama akimwelekea Yesu, alipoona amekufa kwa jinsi ile, akasema, “Kweli huyu mtu alikuwa Mwana wa Mungu.” 40 Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakitazama kwa mbali. Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu (mama yake Yakobo mdogo wa Yose), na Salome. 41 Wakati alipokuwa Galilaya walimfuata na kumtumikia. Na wanawake wengine wengi pia waliambatana naye hadi Yerusalemu. 42 Kulipokuwa jioni, na kwa kuwa ilikuwa siku ya maandalio, siku kabla ya Sabato, 43 Yusufu wa Arimathaya alikuja pale. Alikuwa ni mjumbe wa Baraza anayeheshimiwa mtu anayeutarajia Ufalme wa Mungu. Kwa ujasiri akaenda kwa Pilato, na kuuomba mwili wa Yesu. 44 Pilato akashangazwa kwamba Yesu tayari amekufa; akamwita yule afisa akamwuliza kama Yesu amekufa. 45 Alipopata uhakika kwa afisa kwamba amekufa, alimruhusu Yusufu kuuchukua mwili. 46 Yusufu alikuwa amenunua sanda. Akamshusha toka msalabani, akamfunga kwa sanda, na kumweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika mwamba. Kisha akalivingirisha jiwe mlangoni mwa kaburi. 47 Mariamu Magdalena na Mariamu mama yake Yose waliona sehemu alipozikwa Yesu.