16
1 Wakati sabato ilipokwisha, Mariamu Magdalena na Mariamu mama yake na Yakobo, na Salome, walinunua manukato mazuri, ili waweze kuja na kuupaka mafuta mwili wa Yesu kwa ajili ya maziko.
2 Asubuhi na mapema siku ya kwanza ya juma, walienda kwenye kaburi wakati jua lilipochomoza.
3 Wakisemezana wao kwa wao, “Nani ataliviringisha jiwe kwa ajili yetu ili tuingie kaburini?”
4 Wakati walipotazama, walimuona mtu amekwisha kulivingirisha jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana.
5 Wakaingia kwenye kaburi na wakamwona kijana amevaa joho jeupe, ameketi upande wa kulia, na wakashangazwa.
6 Akawaambia, “Msiogope. Mnamtafuta Yesu, wa Nazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayupo hapa. Tazama mahali pale walipokuwa wamemweka.
7 Nendeni, mkawaambie wanafunzi wake na Petro ya kuwa amewatangulia kuelekea Galilaya. Huko mtamwona, kama alivyokua amewaambia.”
8 Wakaondoka na kukimbia kutoka kwenye kaburi; walitetemeka na walishangazwa. Hawakusema chochote kwa mtu yeyote sababu waliogopa sana.
9 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Mapema katika siku ya kwanza ya juma, baada ya kufufuka, alimtokea kwanza Mariamu Magdalena, ambaye kutoka kwake alimtoa mapepo saba.
10 Aliondoka na kuwaambia wale ambao walikuwa pamoja naye, wakati walipokuwa wakihuzunika na kutoa machozi.
11 Walisikia kwamba ni mzima na ameonekana naye, lakini hawakumwamini.
12 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Baada ya hayo, akajitokeza katika namna tofauti kwa watu wengine wawili, wakati walipokuwa wakitembea kutoka katika nchi.
13 Walienda na kuwaambia wanafunzi wengine waliobaki, lakini hawakuwaamini.
14 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Yesu baadaye akajitokeza kwa wale kumi na mmoja walipokuwa wameegama katika meza, na akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo, kwa sababu hawakuwaamini wale waliomwona baada ya kufufuka kutoka kwa wafu.
15 Akawaambia, “ Enendeni ulimwenguni mwote, na kuhubiri injili kwa viumbe vyote.
16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokolewa, na yule asiyeamini atahukumiwa.
17 (Zingatia: Nakala za kale hazina Marko 16: 9-20) Ishara hizi zitaambatana na wote waaminio. Kwa jina langu watatoa pepo. Watasema kwa lugha mpya.
18 Watashika nyoka kwa mikono yao, na hata wakinywa kitu chochote cha kufisha hakitawadhuru. Wataweka mikono kwa wagonjwa, nao watakuwa wazima”.
19 Baada ya Bwana kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
20 Wanafunzi wakaondoka na kuhubiri kila mahali, wakati Bwana akifanya kazi nao na kulithibitisha neno kwa miujiza na ishara zikifuatana nao.