3
1 Na tena aliingia ndani ya sinagogi na mle palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza.
2 Baadhi ya watu walikuwa wakimfuatilia kwa ukaribu kuona kama atamponya siku ya Sabato ili kwamba wamshitaki.
3 Yesu alimwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “ Inuka na usimame katikati ya umati huu.”
4 Kisha akawaambia watu, “Je ni halali kutenda tendo jema siku ya Sabato au kutenda yasiyo haki; kuokoa maisha, au kuua?” Lakini walibaki kimya.
5 Akawaangalia kwa hasira, akihuzunika kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, na akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako”. Akaunyoosha na Yesu akamponya mkono wake.
6 Mafarisayo wakaenda nje na mara wakafanya njama pamoja na Maherode dhidi yake ili kumuua.
7 Kisha Yesu, pamoja na wanafunzi wake, walienda baharini, na umati mkubwa wa watu uliwafuata ukitokea Galilaya na Uyahudi
8 na kutoka Yerusalemu na kutoka Idumaya na mbele ya Yorodani na jirani ya Tiro na Sidoni, umati mkubwa, uliposikia kila kitu alichokuwa anakifanya, walikuja kwake.
9 Na aliwaambia wanafunzi wake kuandaa mtubwi mdongo kwa ajili yake kwa sababu ya umati, ili kwamba wasije wakamsonga.
10 Kwa kuwa aliponya wengi, ili kila mtu aliyekuwa na mateso alikuwa na shauku ya kumfikia ili amguse.
11 Popote roho wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kulia, na walisema, “Wewe ni Mwana wa Mungu”.
12 Aliwaamuru kwa msisitizo wasifanye ajulikane.
13 Alienda juu ya mlima, na akawaita aliowataka, na wakaenda kwake.
14 Akawachagua kumi na wawili (aliowaita mitume), ili kwamba wawe pamoja naye na aweze kuwatuma kuhubiri,
15 na kuwa na mamlaka ya kutoa mapepo.
16 Na akawachagua kumi na wawili: Simoni, aliyempa jina la Petro,
17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana ndugu yake Yakobo, aliyepewa jina la Bonagesi, hao ni, wana wa ngurumo,
18 na Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo,
19 na Yuda Iskariote, ambaye atamsaliti.
20 Kisha alienda nyumbani, na umati wa watu wakaja pamoja tena, hata wasiweze kula hata mkate.
21 Familia yake waliposikia habari hiyo, walienda kumkamata, kwani walisema, “ Amerukwa na akili”.
22 Waandishi waliokuja kutoka Yerusalemu walisema, “ Amepagawa na Beelzebuli,” na, “ Kwa mtawala wa mapepo anatoa mapepo”.
23 Yesu aliwaita kwake na kusema nao kwa mifano, “ Jinsi gani Shetani aweza kumtoa Shetani?
24 Kama ufalme ukigawanyika wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.
25 Kama nyumba ikigawanyika yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.
26 Kama Shetani atainuka kinyume chake mwenyewe na kugawanyika, hawezi kusimama, na atakuwa amefika mwisho wake.
27 Lakini hakuna hata mmoja awezaye kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake bila kumfunga mwenye nguvu kwanza, na kisha kukusanya kilichomo nyumbani.
28 Kweli nawambieni, dhambi zote za wana wa watu zitasamehewa, pamoja na kufuru ambazo wanatamka,
29 lakini yeyote atakaye mkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, bali ana hatia ya dhambi ya milele”.
30 Yesu alilisema hili kwa sababu walikuwa wakisema, “Ana roho chafu”.
31 Kisha mama yake na ndugu zake walikuja na kusimama nje. Wakamtuma mtu, kumwita.
32 Na umati wa watu uliokuwa umekaa karibu naye wakamwambia, “mama yako na ndugu zako wako nje, na wanakutafuta wewe”.
33 Aliwajibu, “Ni nani mama yangu na ndugu zangu?”
34 Aliwaangalia waliokuwa wamekaa wamemzunguka, na akasema, “Tazama, hawa ni mama zangu na ndugu zangu!
35 Yeyote afanyaye mapenzi ya Mungu, mtu huyo ni ndugu yangu, na dada yangu, na mama yangu”.