4
1 Tena alianza kufundisha kandokando ya bahari. Na umati mkubwa ulikusanyika ukamzunguka, akaingia ndani ya mtumbwi baharini, na kukaa. Umati wote walikuwa pembeni mwa bahari ufukweni.
2 Na akawafundisha mambo mengi kwa mifano, na akasema kwao kwa mafundisho yake.
3 Sikilizeni, mpanzi alienda kupanda.
4 Alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu zilianguka njiani, na ndege wakaja wakazila.
5 Mbegu zingine zilianguka kwenye mwamba, ambako hapakuwa na udongo mwingi. Mara zikanyauka, kwa sababu hazikuwa na udongo wakutosha.
6 Lakini jua lilipochomoza, zilinyauka, na kwa sababu hazikuwa na mzizi, zilikauka.
7 Mbegu ziingine zilianguka katikati ya miiba. Miiba ilikua na ikazisonga, na hazikuzaa matunda yeyote.
8 Mbegu zingine zilianguka kwenye udongo mzuri na zikazaa matunda wakati zikikua na kuongezeka, zingine zilizaa mara thelathini zaidi, na zingine sitini, na zingine mia”.
9 Na akasema, “Yeyote mwenye masikio ya kusikia, na asikie!”
10 Yesu alipokuwa peke yake, wale waliokuwa karibu naye na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano.
11 Akasema kwao, “Kwenu mmepewa siri za ufalme wa Mungu. Lakini kwa walio nje kila kitu ni mifano,
12 ili wakitazama, ndiyo hutazama, lakini hawaoni, na kwa hiyo wanaposikia ndiyo husikia, lakini hawaelewi, amasivyo wangegeuka na Mungu angeliwasamehe.”
13 Na akasema kwao, “Je hamuelewi mfano huu? Mtawezaje kuelewa mifano mingine?.
14 Mpanzi alipanda neno.
15 Baadhi ni wale walioanguka pembeni mwa njia, mahali neno lilipopandwa. Na walipolisikia, mara Shetani akaja na kulichukua neno ambalo lilipandwa ndani yao.
16 Na baadhi ni wale waliopandwa juu ya mwamba, ambao, wanapolisikia neno, kwa haraka wanalipokea kwa furaha.
17 Na hawana mizizi yoyote ndani yao, lakini huvumilia kwa muda mfupi. Halafu tabu na masumbufu vinapokuja kwa sababu ya neno, mara hujikwaa.
18 Na wengine ni wale waliopandwa katika miiba. Wanalisikia neno,
19 lakini masumbufu ya dunia, udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine, huwaingia na kulisonga neno, na linashindwa kuzaa matunda.
20 Kisha kuna wale ambao wamepandwa kwenye udongo mzuri. Wanalisikia neno na kulipokea na huzaa matunda: baadhi thelathini, na baadhi sitini, na baadhi mia moja.”
21 Yesu akawaambia, “ Je huwa unaleta taa ndani ya nyumba na kuiweka chini ya kikapu, au chini ya kitanda? Huileta ndani na kuiweka juu ya kiango.
22 Kwa kuwa hakuna chochote kilichojificha ambacho hakitajulikana, na hakuna siri ambayo haitawekwa wazi.
23 Akiwapo mwenye masikio ya kusikia, na asikie!”
24 Akawaambia, “ Iweni makini kwa kile mnachokisikia, kwa kuwa kipimo mpimacho, ndicho mtakachopimiwa, na itaongezwa kwenu.
25 Kwa sababu yeye aliyenacho, atapokea zaidi, na yule asiyenacho, kutoka kwake vitachukuliwa hata vile alivyonavyo.”
26 Na akasema, “Ufalme wa Mungu umefananishwa na mtu aliyepanda mbegu katika udongo.
27 Alipolala usiku na kuamka asubuhi, na mbegu zikachipuka na kukua, ingawa hajui ilivyotokea.
28 Dunia hutoa mbegu yenyewe; kwanza majani, halafu maua, halafu mbegu zilizo komaa.
29 Na wakati mbegu itakapokua imeiva mara hupeleka mundu, kwa sababu mavuno yamewadia.”
30 Na akasema, “tuufananishe ufalme wa Mungu na kitu gani, au tutumie mfano gani kuuelezea?.
31 Ni kama mbegu ya haradali, ambapo ilipopandwa ni ndogo sana kuliko mbegu zote duniani.
32 Hata, wakati imepandwa, inakuana kuwa kubwa zaidi ya mimea yote ya bustani, na inafanya matawi makubwa, hata ndege wa mbinguni huweza kufanya viota vyao kwenye kivuli chake.”
33 Kwa mifano mingi alifundisha na alisema neno kwao, kwa kadiri walivyoweza kuelewa,
34 na hakusema nao bila mifano. Lakini wakati alipokuwa peke yake, akawaelezea kila kitu wanafunzi wake.
35 Katika siku hiyo, wakati wa jioni ulipowadia, akasema kwao, “Twendeni upande wa pili”.
36 Hivyo wakauacha umati, wakamchukua Yesu, wakati huo tayari alikuwa ndani ya mtumbwi. Mitumbwi mingine ilikuwa pamoja naye.
37 Na upepo mkali wa dhoruba na mawimbi yalikuwa yakiingia ndani ya mtumbwi na mtumbwi tayali ulikuwa umejaa.
38 Lakini Yesu mwenyewe alikuwa kwenye shetri, amelala kwenye mto. Wakamwamsha, wakisema, “Mwalimu, haujali sisi tunakufa?”
39 Na akaamka, akaukemea upepo na akaiambia bahari, “'Iwe shwari, amani”. Upepo ukakoma, na kulikuwa na utulivu mkubwa.
40 Na akasema kwao, “Kwa nini mnaogopa? Je hamna imani bado?”
41 Walijawa na hofu kubwa ndani yao na wakasemezana wao kwa wao, “ Huyu ni nani tena, kwa sababu hata upepo na bahari vya mtii?”.