7
Mafarisayo na baadhi ya waandishi ambao walikuwa wametokea Yerusalemu walikusanyika kumzunguka yeye. Na waliona kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikula mkate kwa mikono najisi; ambayo haikuoshwa. (kwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali mpaka wameosha mikono yao vizuri; wanashikilia utamaduni wa wazee. Wakati Mafarisayo wanaporudi kutoka mahali pa soko, hawali mpaka wameoga kwanza. Na kuna sheria zingine ambazo wanazifuata kabisa, ikiwa ni pamoja na kuosha vikombe, masufuria, vyombo vya shaba, na hata viti vinavyotumika wakati wa chakula.) Mafarisayo na waandishi walimuuliza Yesu, “ Kwa nini wanafunzi wako hawaishi kulingana na tamaduni za wazee, kwani wanakula mkate pasipo kunawa mikono?” Lakini yeye aliwaambia, “Isaya alitabiri vizuri kuhusu ninyi wanafiki, aliandika, 'Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali na mimi. Wananifanyia ibaada zisizo na maana, wakifundisha sheria za wanadamu kama mapokeo yao.' Mmeiacha sheria ya Mungu na kushikilia kwa wepesi tamaduni za wanadamu.” Na akasema kwao, “Mmeikataa amri ya Mungu kwa urahisi ili kwamba mtunze tamaduni zenu! 10 Kwa kuwa Musa alisema, 'mheshimu baba yako na mama yako,' na 'Yeye asemaye mabaya juu ya baba yake au mama yake hakika atakufa.' 11 Lakini mnasema, 'kama mtu akisema kwa baba yake au mama, “Msaada wowote ambao mngepokea kutoka kwangu ni hazina ya Hekalu,”' (hiyo ni kusema kwamba, 'imetolewa kwa Mungu') 12 hivyo haumruhusu kufanya jambo lolote kwa ajili ya baba au mama yake. 13 Mnaifanya amri ya Mungu kuwa bure kwa kuleta tamaduni zenu. Na mambo mengi ya jinsi hiyo mnayoyafanya.” 14 Aliwaita makutano tena na kuwaambia, “Mnisikilize mimi, ninyi nyote, na mnielewe. 15 Hakuna chochote kutoka nje ya mtu ambacho chaweza kumchafua mtu kiingiapo kwake. Bali ni kile kimtokacho mtu ndicho kimchafuacho. 16 (Zingatia: mstari huu, “kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia, na asikie” haumo kwenye nakala za kale). 17 Yesu alipowaacha makutano na kuingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu mfano huo. 18 Yesu akasema, “Na ninyi pia bado hamjaelewa? Hamuoni kwamba chochote kimuingiacho mtu hakiwezi kumchafua, 19 kwa sababu hakiwezi kwenda kwenye moyo wake, lakini kinaingia katika tumbo lake na kisha kinapita kwenda chooni.” Kwa maelezo haya Yesu alivifanya vyakula vyote kuwa safi. 20 Alisema, “Ni kile ambacho kinamtoka mtu ndicho kimchafuacho. 21 Kwa kuwa hutoka ndani ya mtu, nje ya moyo, hutoka mawazo maovu, zinaa, wizi, mauaji, 22 uasherati, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, kujamiiana, wivu, kashfa, majivuno, ujinga. 23 Maovu haya yote yanatoka ndani, ndiyo yale yamchafuayo mtu.” 24 Aliamka kutoka pale na kuondoka kwenda katika mkoa wa Tiro na Sidoni. Aliingia ndani na hakutaka mtu yeyote ajue kuwa alikuwa hapo, lakini haikuwezekana kumficha. 25 Lakini ghafla mwanamke, ambaye mtoto wake mdogo alikuwa na roho mchafu, alisikia habari zake, akaja, na akaanguka miguuni pake. 26 Mwanamke huyo alikuwa Myunani, wa kabila la Kifoeniki. Alimsihi yeye amfukuze pepo kutoka kwa binti yake. 27 Yesu akamwambia mwanamke, “Waache watoto walishwe kwanza, kwa kuwa sio sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuwatupia mbwa.” 28 Lakini mwanamke akamjibu na kusema, “Ndiyo Bwana, hata mbwa chini ya meza hula mabaki ya chakula cha watoto.” 29 Akamwambia, “Kwa kuwa umesema hivi, uko huru kwenda. Pepo ameshamtoka binti yako.” 30 Mwanamke alirudi nyumbani kwake na akamkuta binti yake amelala kitandani, na pepo alikuwa amemtoka. 31 Yesu alitoka tena nje ya mkoa wa Tiro na kupitia Sidoni kuelekea Bahari ya Galilaya mpaka kanda ya Dikapolisi. 32 Na wakamletea mtu aliyekuwa kiziwi na alikuwa hawezi kuzungumza vizuri, walimsihi Yesu aweke mikono juu yake. 33 Alimtoa nje ya kusanyiko kwa siri, na akaweka vidole vyake kwenye masikio yake, na baada ya kutema mate, aligusa ulimi wake. 34 Alitazama juu mbinguni, akahema na kumwambia, “Efata,” hiyo ni kusema “funguka!” 35 Na muda ule ule masikio yakafunguka, na kilichokuwa kimezuia ulimi kiliharibiwa na akaweza kuongea vizuri. 36 Na aliwaamuru wasimwambie mtu yeyote. Lakini kadri alivyowaamuru, ndivyo walivyotangaza habari hizo kwa wingi. 37 Hakika walishangazwa, na kusema, “Amefanya kila kitu vizuri. Hata amewafanya viziwi kusikia na mabubu kuongea.”