8
1 Katika siku hizo, kulikuwa tena na umati mkubwa, na hawakuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia,
2 “Ninauhurumia umati huu, wameendelea kuwa nami kwa siku tatu na hawana chakula.
3 Nikiwatawanya warudi majumbani kwao bila kula wanaweza wakazimia njiani kwa njaa. Na baadhi yao wametoka mbali sana.”
4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwashibisha watu hawa katika eneo hili lililoachwa?”
5 Akawauliza, “mna vipande vingapi vya mikate?” Wakasema, “Saba”.
6 Aliuamuru umati ukae chini. Akachukua mikate saba, akamshukuru Mungu, na kuivunja. Akawapa wanafunzi wake waiweke mbele yao, nao wakaiweka mbele ya umati.
7 Pia walikuwa na samaki wadogo wachache, na baada ya kushukuru, aliwaamuru wanafunzi wake wawagawie hivi pia.
8 Walikula na wakatosheka. Na walikusanya vipande vilivyo baki, vikapu vikubwa saba.
9 Walikaribia watu elfu nne. Na aliwaacha waende.
10 Mara aliingia kwenye mashua na wanafunzi wake, na wakaenda katika ukanda ya Dalmanuta.
11 Kisha Mafarisayo walitoka nje na kuanza kubishana naye. Walitaka awape ishara kutoka mbinguni, kwa kumjaribu.
12 Akatafakari kwa kina moyoni mwake akasema, “Kwa nini kizazi hiki kinatafuta ishara? Nawaambia ninyi kweli, hakuna ishara itakayotolewa kwa kizazi hiki.”
13 Kisha akawaacha, akaingia ndani ya mashua tena, akaondoka kuelekea upande mwingine.
14 Wakati huo wanafunzi walisahau kuchukua mikate. Hawakuwa na mikate zaidi ya kipande kimoja kilichokuwa kwenye mashua.
15 Aliwaonya na kusema, “Muwe macho na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.
16 Wanafunzi wakasemezana wao kwa wao, “Ni kwa sababu hatuna mikate.”
17 Yesu alilitambua hili, na akawaambia, “Kwa nini mnasemezana kuhusu kutokuwa na mikate? Hamjajua bado? Hamuelewi? Mioyo yenu imekuwa miepesi?
18 Mna macho, hamuoni? Mna masikio, hamsikii? Hamkumbuki?
19 Nilipoigawanya mikate mitano kwa watu elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vilivyo jaa vipande vya mikate?” Wakamjibu, “kumi na mbili.”
20 “Na nilipoigawanya mikate saba kwa watu elfu nne, mlichukua vikapu vingapi?”
21 Wakasema, “Saba.” Akawaambia, “Bado hamuelewi?”
22 Wakaja Bethsaida. Watu hao walimleta kwa Yesu mtu kipofu na wakamsihi Yesu amguse.
23 Yesu akamshika kwa mkono yule kipofu, na kumwongoza nje ya kijiji. Alipotema mate juu ya macho yake na kunyosha mikono yake juu yake, alimuuliza, “Unaona chochote?”
24 Alitazama juu na kusema, “Naona watu wanaonekana kama miti inatembea.”
25 Ndipo akanyosha tena mikono yake juu ya macho yake, mtu yule akafungua macho yake, aliona tena, na akaona kila kitu vizuri.
26 Yesu alimwacha aende nyumbani na akamwambia, “Usiingie mjini.”
27 Yesu aliondoka na wanafunzi wake kwenda vijiji vya Kaiseria ya Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi, “Watu wanasema mimi ni nani?”
28 Wakamjibu wakasema, “Yohana mbatizaji. Wengine wanasema, 'Eliya' na wengine, 'Mmoja wa Manabii.”
29 Akawauliza, “Lakini ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro kamwambia, “Wewe ni Kristo.”
30 Yesu akawaonya wasimwabie mtu yeyote kumuhusu Yeye.
31 Na akaanza kuwafundisha ya kuwa Mwana wa Adamu lazima ateseke kwa mambo mengi, na atakataliwa na viongozi na makuhani wakuu, na waandishi, na atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka.
32 Alisema haya kwa uwazi. Ndipo Petro akamchukua pembeni na akaanza kumkemea.
33 Lakini Yesu aligeuka na kuwatazama wanafunzi wake na akamkemea Petro na kusema, “Pita nyuma yangu Shetani! Hujali mambo ya Mungu, isipokuwa mambo ya watu.”
34 Kisha akauita umati na wanafunzi wake pamoja, na kuwaambia, “Kama kuna mtu anataka kunifuata, ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake, na anifuate.
35 Kwa kuwa yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili, atayaokoa.
36 Inamfaidia nini mtu, kupata ulimwengu wote, na kisha kupata hasara ya maisha yake?
37 Mtu anaweza kutoa nini badala ya maisha yake?
38 Yeyote anioneaye aibu na maneno yangu katika kizazi hiki cha wazinzi na kizazi cha wenye dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea aibu atakapokuja katika ufalme wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.